MIPAKA NA ENEO:

Wilaya ya Karagwe inapakana na Wilaya ya Kyerwa Kaskazini, Nchi ya Rwanda upande wa Kusini Magharibi, Wilaya ya Ngara upande wa Kusini na       Wilaya ya Missenyi, Bukoba na Muleba upande wa Mashariki. Wilaya ina      eneo la kilomita za mraba 4,500, kati ya hizo kilomita za mraba 4,342          ni eneo la nchi kavu na kilomita za mraba 158 ni eneo la maji.           Mwinuko wa ardhi kutoka usawa wa bahari ni mita 1500 hadi mita   1800.  Hali ya hewa kwa ujumla ni joto la wastani wa 26ºC.  Mvua      zinanyesha kwa wastani wa milimita 1,040 hadi 1,200 kwa mwaka kati   ya mwezi Septemba na Januari na kati ya mwezi Machi na mwezi Mei.

MUUNDO WA WILAYA- KIUTAWALA

Wilaya kwa sasa inaundwa na  Tarafa 5, Kata 23, Vijiji 77, Vitongoji 630,  Idadi ya kaya ni 76,425, na wastani wa watu kwa kila kaya ni      4.6. Aidha tunalo jimbo moja la Uchaguzi la Karagwe.

ENEO NA UTAWALA KWENYE MAMLAKA YA MJI MDOGO WA KAYANGA:

Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kayanga ina umri wa miaka 12 tangu kutangazwa katika gazeti la serikali Na. 352 la tarehe 17/09/2004, aidha imeundwa kwa kufuata Sheria ya Serikali za Mitaa Namba 7/1982 na namba 8/1982 na imeanzishwa kwa kifungu namba 13 cha Sheria ya Serikali za Mitaa. Kisheria siyo sehemu ya Halmashauri ya Wilaya. Mji huu una umri wa miaka mitano tangu kuzinduliwa na Baraza la         Madiwani la Halmashauri Aprili mwaka 2010.

ENEO NA UTAWALA:

Mamlaka hii ina ukubwa wa M2. 184,500 na inaundwa na Tarafa moja      ya Bugene, Kata tano na vilivyokuwa vijiji vinane vyenye    vitongoji/mitaa 86 ambazo ni:- Ndama, Kayanga, Bugene, Nyakahanga      na Ihanda. Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 Mamlaka inao wakazi      wapatao 58,827.Ofisi ya muda ya Mamlaka ya Mji Mdogo iko eneo la       Machinjioni – Kayanga. Mamlaka inayo maeneo mawili ambayo ni     maarufu kwa biashara ambayo ni Kayanga na Omurushaka.

IDADI YA WATU

Kutokana na takwimu za Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Wilaya ya Karagwe ina jumla ya watu  332,020.  Kati ya hao 163,864   (wanaume) na 168,156 (wanawake).Maoteo ya watu kwa mwaka 2016      ni 372,242. Kati ya hao, wanawake ni 189,844 na wanaume ni 182,399.       Aidha idadi ya kaya nayo imeongezeka toka kaya 72,836 mwaka 2012         hadi kaya 76,425 mwaka 2016.

Ongezeko la watu ni asilimia 2.9 kwa mwaka. Msongamano wa watu katika kila kilomita moja ya mraba inakaliwa na watu 74 wakati wastani wa kitaifa ni 49. Aidha idadi ya makundi mbalimbali ya kijamii ni watoto wenye umri chini ya miaka 5 ambao idadi yao ni 60,445, miaka 5 - 17 ni 116,691, Vijana wenye umri wa miaka 18 – 45 ni 116,652, watu wenye umri wa kuanzia miaka 46 – 59 ni 21,653 na wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea ni 16,579. Pia Wilaya ina makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu ambao ni walemavu   wasioona 52, wasiosikia ni 16, wenye ulemavu wa ngozi ni 22 na wenye ulemavu wa viungo ni 1,237. 

HALI YA UCHUMI NA MAENDELEO YA WILAYA

Juhudi zinaendelea kufanyika katika sekta kuu za uzalishaji, huduma za jamii na sekta za kiuchumi ili kuboresha hali ya maisha ya wananchi. Shughuli kuu ni kilimo cha Kahawa kama zao la biashara, Ndizi na Maharage kama chakula na biashara na ufugaji hususani ng'ombe na mbuzi.

Mchango wa kila sekta katika maendeleo ya uchumi ni Kilimo 80%, shughuli za biashara 4%, watumishi (kazi za ofisini) 3%, ufugaji 10%,   shughuli nyingine ndogo ndogo 3%.

Pato la mwananchi kwa mwaka (Per-Capita Income) limeongezeka     kutoka Shs. 150,000/= kwa mwaka 2005 hadi kufikia Shs. 475,000/=    kwa mwaka 2012 (Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi 2012). Na        sasa linakadiriwa kufikia Tsh. 760,000 kwa mwaka 2016.

Wilaya ya Karagwe inazo Asasi zisizo za kiserikali (AZAKI) inazoshirikiana nazo katika shughuli za kiuchumi na kijamii.  Asasi hizo ni KCBRP, TUMAINI FUND, ELCT-HIV/AIDS CONTROL PROGRAMME, WOMEDA, SAWAKA, KARADEA, KADERES, KADENVO, NEKIMAMA, FORUM SYD, KAWOSA SACCOS, WAESA SACCOS, VITUSA, MAVUNO na WORLD VISION.

          Asasi hizo zinatoa huduma kwenye jamii kama kutoa mikopo kwa     wajasiriamali,  kutoa huduma za kibenki, kusaidia watoto walio katika   mazingira magumu zaidi kwa kuwalipia ada za shule, kuwasaidia watu     wenye ulemavu, kusaidia wazee, kutoa huduma za kisheria, kusaidia        wanawake na kutoa huduma za kilimo, elimu , afya na maji.

© 2016 Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.Haki zote zimehifadhiwa.

Imesanifiwa na Kutengenezwa na Mtaalam Masuala ya tovuti na Inaendeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.