Na Innocent E. Mwalo.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya, kupitia Mkutano wake wa robo ya tatu iliyoanzia Januari mpaka Machi, 2021, uliofanyika katika Ukumbi wa Vijana Rafiki wa Angaza mnamo Aprili 28/29, umeagiza na kushauri mambo kadhaa yanapaswa kutekelezwa katika Halmashauri hii ili kuongeza tija ya kuwahudumia wananchi wa Karagwe.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya, Mh. Wallace Mashanda, licha ya kupongeza jitihada zilizofikiwa na Halmashauri katika suala nzima la ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo hadi kufikia robo tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021, mwezi Machi, Halmashauri ya Wilaya imeshakusanya mapato hadi kufikia asilimia 88.
Mh. Mashanda aliiasa menejimenti kutokubweteka na mafanikio hayo na alitoa angalizo la kwamba pamoja na mafanikio yaliyofikiwa katika kukusanya mapato, huenda Halmashauri haikukadiria ipasavyo kutokana na wingi wa vyanzo vya mapato ya ndani katika Halmashauri hii.
Aidha kupitia mkutano huo, Mh. Mashanda aliwajulisha wananchi wa Karagwe ya kwamba kwa kipindi cha kuanzia Julai 2020 mpaka Machi 2021 tayari Halmashauri ya Wilaya imepokea kiasi cha takribani bilioni 4.12 ikiwa ni fedha kutoka serikali kuu na wafadhili mbalimbali kwa ajili ya kufadhili shughuli mbalimbali ikiwemo Elimu bure na chakulani mashuleni, fedha za mradi wa TASAF, maboma ya shule ya msingi na miradi mingine zaidi ya 20 ya maendeleo.
Mkutano huu uliotawaliwa na mjadala mkali kutoka kwa wajumbe wa baraza la madiwani hasa katika utelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita ambao ulifanyika mwezi Januari mwaka huu.
Katika mkutano huu, wajumbe kwa mara nyingine tena, baada ya hoja iliyoibuliwa na Mh. Maginus Cheusi ambaye ni Diwani wa Kata ya Kibondo, waliazimia juu ya kuhamasishwa kwa akina mama wajawazito ili waweze kuwa na bima ya afya itakayowawezesha kuwa na uhahika wa matibabu ikilinganishwa na ilivyo sasa ambapo wanawake wengi wanapata vikwazo wakati wa kujifungua kutokana na tatizo la ukosefu wa fedha za kulipia huduma hizo kwa malipo ya tele kwa tele.
Katika hatua nyingine waheshimiwa madiwani kupitia baraza hili waliagiza kutokujitokeza tena kwenye taarifa zinazowasilishwa na kamati za maendeleo ya kata juu ya ukosefu wa uji na chakula cha mchana mashuleni kutokana na wilaya hii kuelekea kwenye msimu wa mavuno ambapo hakutakuwa na kisingizio cha ukosefuwa mahindi yakuchangia huduma hiyo muhimu kwa wanafunzi hao.
Aidha ili kuipa uzito agenda ya lishe na afya kwa ujumla wajumbe waliendelea kusikitishwa na ongezeko wa watoto wenye utapiamlo na kuagiza takwimu za kliniki kwa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano kuwasilishwa katika kila kikao cha kijiji, kamati za maendeleo ya kata pamoja na mikutano mingine inayofanyika katika ngazi ya wilaya ikiwemo mkutano wa baraza la madiwani ili kuipa nguvu ajenda hiyo muhimu kupitia vikao vya maamuzi.
Kupitia mkutano huu wajumbe walienda kusisitiza juu ya kutekelezwa kwa maazimio kadhaa ya mkutano uliopita ambapo pamoja na mambo mengine baraza liliazmia kuwa vituo vya kutolea huduma ya afya yaani zahanati, vituo vya afya na hospitali kutoa huduma za afya kwa masaa yote 24 bila kuwepo na kisingizio chochote.
Katika hatua nyingine wajumbe walionekana kutolikuridhishwa na namna menejimenti ilivyotekeleza azimio la kuhamasisha jamii juu ya kujiunga na bima ya afya iliyoboreshwa ambapo wajumbe waliazimia uboreshwaji wa huduma hiyo kwenye ngazi ya kata na vijiji.
Mjadala mwingine mkali katika mkutano huu, ulihusu marejesho ya mikopo ambayo hutolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu ambapo madiwani waliendelea kushikilia azimio lao lilipitishwa kwenye mkutano wa baraza la Januari 2021 ambapo iliazimiwa kuwa kata zenye madeni madeni makubwa ya mikopo ya kuanzia milioni kumi ambayo haijareshwa, ikiwemo kata ya Kayanga ambayo inadaiwa jumla ya milioni 47 kutokupewa tena mikopo hiyo.
Katika hatua nyingine mkutano wa baraza la madiwani uliipokea na kuipongeza timu ya Nyaishozi FM ya wilayani hapa ambayo imefuzu kuingia ligi ngazi ya daraja la pili kwenye mashindano yaliyofanyikia mkoani Lindi ambapo mabingwa hawa ni wawakilishi pekee wa mkoa wa Kagera.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.