MADIWANI 32 KARAGWE DC WAIANZA SAFARI YA UTUMISHI KWA WANANCHI (2025 - 2030) RASMI LEO.

Jumla ya waheshimiwa madiwani 32 wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe wamekabidhiwa rasmi Mamlaka ya kuwatumikia Wananchi wa Wilaya hiyo, baada ya kuapishwa kiapo cha uadilifu wa Umma mbele ya Hakimu mkazi Mkuu wa Mahakama ya mwanzo Mhe. Flora Haule na mbele ya Afisa Tawala wa Wilaya hiyo Ndg. Rasul Shandala ambaye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo wa kwanza uliofanyika leo Tarehe 02/12/2025, katika ukumbi wa Halmashauri (Angaza).

Aidha, Kupitia Mkutano huo wa Kwanza Waheshimiwa madiwani walipata nafasi ya kufanya Uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, pamoja na kuunda Kamati mbalimbali za Halmashauri ambapo Diwani wa Kata ya Chanika Mhe. Longino W. Rwenduru ameteuliwa kuwa Mwenyekiti na Diwani Kata ya Rugu Mhe. Adrian Kobushoke kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Karagwe Mhe; Innocent Bashungwa amewashukuru Wananchi kwa kuendelea kumuamini yeye na Madiwani na kuongeza kuwa, kupitia baraza hilo kipaumbele chao kiwe ni kuhakikisha wanatatua changamoto na kero walizopokea kutoka kwa Wananchi kipindi walipopita kuomba kura Vilevile alisema kuwa angependa Wilaya ya Karagwe iwe moja kati ya Wilaya ambazo zinatekeleza maagizo ya Rais ya siku 100 kwa wakati.

Kwaupande wake, Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe; Julius Kalanga Laizer amewashukuru Wananchi wa Karagwe kuendelea kudumisha amani na amewasisitiza kujiepusha na viashiria vya uvunjifu wa amani. Pia amesisitiza kuhakikisha ahadi za Rais za siku 100 zinatekelezwa ikiwemo Bima kwa wote na kuhakikisha miradi inasimamiwa vizuri na inatekelezwa kwa wakati.
Vilevile, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Bi.Happiness Msanga aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Halmashauri zilizofanyika kwa kipindi ambacho Baraza la Madiwani lilivunjwa ambapo Waheshimiwa Madiwani walimpongeza Mkurugenzi Mtendaji kwa kusimamia shughuli hizo vyema na kwa weledi pia walipata nafasi ya kuhoji na kupatiwa majibu papo kwa papo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mhe; Longino Rwenduru alifunga Mkutano huo kwa kusisitiza umuhimu wa kusimamia mapato na matumizi ya Halmashauri pamoja na ushirikiano ili kufanikisha malengo kwa wakati.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.