DC LAIZER ATAKA UTAMADUNI WA WANAFUNZI KUPANDA MITI WANAPOANZA SHULE KUENDELEZWA.

Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. Julius Kalanga Laizer amewataka Maafisa Elimu na Wakuu wa Shule kuhakikisha wanaendeleza utamaduni wa Wanafunzi kupanda miti wanapoanza shule na kuendelea kuusimamia kipindi chote watakachokuwa eneo hilo lengo likiwa ni kutunza na kuboresha Mazingira ya shule yao pamoja na kutengeneza historia zao binafsi na shule hiyo.
Wito huo umetolewa mapema leo Januari 31, 2026 katika Shule ya Sekondari Omorushaka ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ilihitimisha wiki ya upandaji miti ambayo ni sehemu ya Kumuunga mkono Kiongozi na Mdau wa Kulinda na Kutunza Mazingira Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye Januari 27 aliadhimisha Siku yake ya kuzaliwa kwa kauli mbiu isemayo “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti” pamoja na kuongoza zoezi la upandaji miti ya matunda katika eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

“Kupanda miti ni jambo moja na kuitunza miti hii ni jambo lingine hivyo nikuombe mwalimu mkuu uisimamie hii miti 500 tuliyopanda leo ikuwe na kustawi. Tumeamua kupanda miti kwenye shule hii kama sehemu ya kuenzi na kuheshimu juhudi za Dkt.Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuboresha Sekta ya Elimu kwenye Wilaya yetu ikiwemo kutujengea Shule mpya, Tunamtia moyo na kumpongeza kwa Kazi ambayo wote tunaiona Shule nzima hii ni mpya si jambo dogo, Tunamshukuru sana” Alisema Mhe.Laizer

Naye, Afisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Bi.Dotto Massanja amesema kuwa Halmashauri hiyo inaunga mkono kauli ya Uzalendo ni pamoja na kupanda miti na kutunza mazingira kwa kuhakikisha inaendelea kutoa elimu kwa Wananchi kujijengea tabia ya kupanda miti kwenye maeneo yao hasa ya matunda na kuacha kukata miti hovyo pia amesema kuwa wameamua kuchagua Shule hiyo ili kuijengea mazingira ya kuvutia na kutengeza vivuli ambavyo watoto watavitumia kujisomea.

Kwa upande wake, Mwanafunzi wa Kidato cha nne Shule ya Sekondari Omorushaka Bi. Neema Renatus ameishukuru Serikali kwa kuichagua shule yao kwaajili ya zoezi hilo kwasababu kupindi cha kiangazi Wanafunzi walikosa maeneo yenye vivuli kwaajili ya kupumzika na kujisomea anaamini miti hiyo itamaliza changamoto hiyo pia itasaidia kwenye uzalishaji wa hewa ya oksijeni na kupunguza hewa ya ukaa pamoja na kupendezesha Mazingira ya shule yao.

Hata hivyo, Mhe.Laizer amewapongeza Wananchi wa Wilaya ya Karagwe kwa kushiriki zoezi la upandaji miti kwa wiki nzima kwenye maeneo tofauti tofauti hadi siku ya leo (Kilele) pia ametoa wito kwa Wananchi wa Wilaya ya Karagwe kuendelea kupanda miti majumbani kwao hasa ya matunda ili kuboresha lishe na afya ya familia, kuimarisha mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.