Na Innocent E. Mwalo.
Ziara ya kikazi aliyoifanya Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mh. Eng. Kundo Andrea Mathew (MB), Wilayani Karagwe mnamo Tarehe 1/8/2021, imemalizika kwa mafanikio makubwa kutokana na ahadi mbalimbali alizozitoa kwa wananchi wa Karagwe ikiwemo ahadi ya uimarishaji wa hali ya upatikanaji wa huduma za simu pamoja na usikivu wa matangazo ya redio.
Kwa nyakati tofauti, akiwa katika maeneo ya vijiji vya Ahakishaka na Nyakaiga katika kata za Nyabiyonza na Kibondo, Mh. Kundo alitembelea na kukagua miradi wa ujenzi wa minara ya simu na mnara kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa matangazo ya redio pamoja na kuzungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika kwenye maeneo hayo.
Katika eneo la Ahakishaka wananchi waliopata fursa ya kuuliza maswali pamoja shukrani ambazo wananchi walitoa kwa ziara hiyo ya naibu waziri huku wakitanabaisha kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa waziri kufunga safari kutoka makao ya Halmashauri ya wilaya umbali wa kilomita 40 na kufika katika maeneo hayo kwa ziara ya kikazi kama ilivyofanywa na waziri huyo.
‘’Mh. Waziri katika kata ya Nyabiyonza tatizo la kukosekana kwa matangazo ya redio za hapa nchini ni kubwa, wananchi wote unaowaona hapa wanapata matangazo kupitia redio za nchi za Rwanda na Burundi’’, alisisitiza Mh. Thomas Rwentabaza, Diwani wa kata hiyo.
Akijibu hoja hiyo pamoja na zile za kufanana na hizo zilizotolewa Dawson Yustice, na Greygory Ludovick kutoka katika kijiji cha Ahakishaka pamoja na Theonest Peter, Jackson Kazungu na Eradius Mnubi wa kijiji cha Nyakaiga juu ya changamoto ya mitandao ya simu, upatikanaji wa mitandao ya simu, changamoto ya miktaba ambayo makampuni ya simu wanansainiana na wananchi au vijiji vinasainia ambapo miradi hiyo inakuwa inatekelezwa.
Maagizo ya Mh. Kundo kwa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mh. Julieth Binyura, ilikuwa ni pamoja na Mkuu wa wilaya huyu kuhakikisha anaelekeza vyombo vyake vya ulinzi na usalama ili katika kila palipo na mnara wa simu pajengwe choo na taa inayowaka juu ya mnara pamoja na kuhakikisha kila mahala panapojengwa minara na huduma za mawasiliano basi mkuu wa wilaya apate taarifa kabla ya kuanza utekelezwaji wa mradi huo.
Aidha maagizo mengine yalikwenda kwa ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ambapo Mh. Kundo aliagiza kuhakikisha suala la ulipaji wa ushuru wa utoaji wa huduma ili wananchi na serikali za vijiji vinavyokuwa vinatoa ardhi kwenye maeneo inapojengwa minara hiyo waweze kunufaika nayo.
‘’Mkurugenzi Mtendaji nikuagize uhakikishe mikataba yote iliyoingiwa na makampuni ya simu inafumuliwa maana kwa jinsi nilivyoona hapa Nyakaiga na kule Ahakishaka ni dhahiri mikataba hii ina walakini mkubwa kutokana na malalamiko haya niliyoyapata kwa wananchi katika maeneo haya ya ziara yangu’’, alisisitiza Mh. Kundo.
Mh. Kundo alisisitiza juu ya umuhimu wa kuondoa vishoka na kufumuliwa kwa mikataba hiyo ili fedha inalipwa na makampuni hayo iwanufaishe wananchi hao wa vijiji hivyo na kuahidi kurudi kwa ziara nyingine kwa ajili ya kushughulikia changamoto hizo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.