YALIYOJIRI KIKAO CHA BARAZA LA MADIWANI
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Baraza la Madiwani Wilayani hapa, linaendelea na kikao chake cha kawaida kwa robo ya tatu ya mwaka wa Fedha 2017/2018, kikao ambacho kinafanyikia katika ukumbi wa Angaza uliopo mjini Kayanga huku kikitarajiwa kudumu kwa takribani wa siku mbili kikiangazia masuala kadhaa wa kadhaa yahusuyo ustawi wa watu wa Karagwe.
Katika siku ya kwanza masuala kadhaa yaliyadiliwa ambapo hapo awali, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, Mh. Wallace Mashanda, katika ufunguzi wa Baraza hilo, aliipongeza Timu ya Menejimenti chini ya Uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashahuri, Mh.Godwin Kitonka kwa kupata hati safi huku akibainisha ya kwamba jambo hilo limefanikiwa kutokana na ushirikiano mkubwa uliofanywa kati ya timu ya menejimenti na Baraza la Madiwani kwa ujumla kupitia kamati zake za kudumu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Mh. Kitonka mapema akimkaribisha Mwenyekiti wa Halmashauri, aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho na wageni waalika pamoja na mambo mengine juu ya kufanya tahadhali ya kuzuia ugonjwa wa Ebola ambao umezuka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC na kwa mujibu wa taatifa za vyombo vya habari inasemekana ugonjwa huo ulikwisha ua takribani watu 21 huko DRC.
“Ugonjwa huu una dalili nyingi lakini zilizo kubwa ni kwamba mgonjwa hupata homa kali ghafla na pia mgonjwa huharisha na kutapika sana”, alisisitiza Mh. Kitonka.
Katika hatua nyingine, kikao hicho kwa kauli moja kilitoa tamko la kudhibiti moto kutokana na musimu wa kiangazi kukaribia huku kwa mara nyingine kikao hicho kikitoa maagizo kwa wananchi kuanza maandalizi ya awali ya kilimo cha mazao ya biashara.
Jambo jingine ambalo lilijitokeza kwenye kikao hicho lilikuwa ni suala la simu akaunti ambao ni mfumo wa kielekroniki utakaotumiwa katika kufanya malipo kwa wakulima wa zao la kahawa ambapo Mratibu wa Mfumo huu kutoka Chama cha Ushirika cha Karagwe, KDCU, Casius Rugemarila aliweza kuwaelezea wajumbe wa kikao hicho juu ya mfumo huo.
Nao wajumbe wa kikao hicho, pamoja na kuunga mkono mfumo huo kuwa mzuri, wito ulitolewa kwa KDCU kuendelea kutafari juu ya kuendelea pia na mfumo wa malipo ya wa papo kwa papo kwani kwa hali halisi sio wakulima wote wanaweza kutumia simu katika shughuli za malipo hayo. Na katika suala hili ilisisitizwa ya kwamba, Halmashauri inao wajibu wa kusimamia kilimo cha kahawa ikiwemo kuratibu uanzishwaji wa vyama vya ushirika.
Katika kujadili taarifa za Mabaraza ya Kata, WDC, wajumbe waliibua masuala kadhaa ambayo ni changamoto kwenye maeneo yao ikiwemo suala la upungufu wa watumishi katika kada za afya na utawala. Ilifafanuliwa ya kwamba kwa sasa serikali imetangaza takribani nafasi 6,000 kwa watumishi wa kada ya afya na mara watakapoajiriwa watumishi hao kipaumbele cha maeneo ambapo kuna upungufu wa watoa huduma hao kitazingatiwa.
Jambo jingine lililojadiliwa kwa msisitizo lilikuwa ni suala la gugu karoti ambao ni mmea unaotajwa kuharibu sana mazao ambapo iliagizwa ya kwamba wananchi wachukue tahadhali ya kung’oa na kuchoma moto gugu hilo pindi mmea unapoonekana kuathiriwa na gugu hilo ili mmea huo usiendelea kuleta madhara kwa mimea mingine iliyo karibu nao.
Aidha masuala mengine yaliyopewa nafasi ya kujadiliwa ilikuwa ni suala la utambuzi wa wazee kwa ajili ya matibabu, agizo kwa wananchi wote juu ya ujenzi na matumizi bora ya ardhi ili kuepuka kukumbana na faini zitakazotozwa kwa wale watakaokaidi agizo hilo.
Katika kikao hicho wajumbe kwa kauli moja waliiomba Wakala wa Barabara, Mjini na Vijijini, TARURA kurejesha miundombinu ya barabara iliyoharibiwa vibaya kutokana na mvua kwenye maeneo yao.
Katika kuhitimisha kikao kwa siku ya kwanza Mh. Wallace Mashanda alitoa wito kwa waheshimiwa madiwani kuwasilisha kwake maandiko kama wakifanikiwa kuandika juu ya namna yeyote ile ya kuboresha ustawi wa wananchi wa Karagwe.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.