Na Innocent E. Mwalo.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Bi. Julieth Binyura, mnamo 10/08/2021, amezindua kikao kazi cha kujenga uelewa kuhusu kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini Tanzanaia (TASAF).
Akizungumza na wawezeshaji waliofika ili kupata mafunzo hayo, Mh. Binyura alisema kuwa madhumuni ya mpango wa kipindi cha pili ni kuwezesha kaya za walengwa kutumia fursa za kuongeza kipato, kuboresha huduma za jamii na kiuchumi, na kuwezesha katika maendeleo ya watoto ambao ni raslmali watu.
Mh. Binyura ameishukuru Serikali ya awamu ya sita na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasan kwa kuendelea kuuboresha mpango huu wa TASAF na kuona tija ya kuzisaidia kaya hizo maskini ili ziweze kunufaika.
Aidha amewataka wawezeshaji kuzingatia mafunzo watakayopatiwa na wataalamu na kwamba wazingatie na kuhakikisha mpango unawafikia walengwa pindi watakapokuwa uko vijijini na wafuate miongozo iliyowekwa na kuwa makini.
“Nitoe rai kwenu wote kuzingatia mafunzo haya na kuhakikisha mnatekeleza mpango kazi huu mtakapokuwa huko vijijini basi mkazingazitie miongozo mliyopewa na kuhakikisha walengwa wote wananufaika na mpango huu”alisema Mh. Binyura.
Akisoma hotuba mbele ya Washiriki wa Mafunzo hayo Afisa Mwezeshaji kutoka wa TASAF Makao Makuu, ndugu Ahmed Mafiu, amesema kuwa kipindi cha awamu ya tatu ya mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAFIII) kinatekelezwa katika Halmashauri zote 184 za Tanzania Bara na Wilaya zote za Zanzibar..
Aidha ameongeza kuwa kipindi cha pili cha awamu ya tatu TASAF kitafika kaya milioni moja laki nne na nusu zenye jumla ya watu zaidi ya million saba nchi nzima.
“Mkazo mkubwa katika kipindi hiki cha pili umewekwa katika kuwezesha kaya zitakazoandikishwa kwenye mpango kufanya kazi ili kuongeza kipato”alisema Mafiu.
Mafiu alisema kuwa kipindi hiki cha pili kitahakikisha kwamba huduma za jamii zinaongezwa na kuboreshwa ili kutoa huduma na kuendeleza rasilmali Watoto hususani katika upatikanaji wa Elimu na Afya.
Akitaja walengwa wa awamu hii ya pili, Mafiu amesema kuwa ni kaya zinazoishi katika hali duni kwenye Vijiji,Mitaa na, Shehia na kwamba wanufaika ndani ya kaya ni Watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaohudhuria kliniki,wanafunzi wa shule za awali,shule za msingi na shule za sekondari,mama wajawazito na mwanakaya mwenye ulemavu.
“Niseme tu kwamba mpango huu unatoa ruzuku za aina mbili,ruzuku ya msingi na ruzuku ya masharti kwa wale ambao wanatakiwa kwenda shuleni na Watoto wanaohudhuria kliniki”alisema Mafiu.
Hata hivyo Lwanda alisema kuwa kuna ajira mpya ambazo pia zitaweza kuwanufaisha mwanakaya mmoja ambaye ataonekana kuwa na uwezo wa kufanya kazi.
Mafiu amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji, Michael Nzyungu kwa kutoa wawewzeshaji wengi na hasa ngazi ya kata ili kuja kushiriki mpango kazi huo.
Naye Mratibu wa TASAF Wilaya ya Karagwe Edius Rwangoga ameshukuru wataalamu hao kwa kuweza kuiweka Wilaya ya Karagwe katika mpango huu kwa awamu nyingine tena na kuwaweka watu wenye ulemavu katika mpango huo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.