Na Innocent Mwalo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mh. Suleimani Jaffo (Mb), mnamo 06/01/2021 alifanya ziara ya kikazi Wilayani Karagwe iliyolenga kukagua na kuangalia maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa wilayani hapa, ambapo pamoja na mambo mengine ameoneshwa kuridhishwa na kufurahishwa sana na utekelezwaji na utunzwaji wa miradi hiyo.
Baadhi ya miradi ambayo Mh. Waziri Jaffo aliitembelea ni pamoja na ujenzi wa vyumba 3 vya madarasa na matundu 6 ya vyoo katika Shule ya Msingi Ihembe ambapo mradi huu umekamilika kwa gharama za shilingi 66, 600,000.00 ikiwa ni fedha iliyotolewa kwa ufadhili wa serikali kupitia Programu ya Lipa Kulingana na matokeo (EP4R).
Huku akioneshwa kuridhishwa sana na utekelezaji na utunzwaji wa mradi huu ambao ulizinduliwa nae mnamo mwaka 2018, Mh. Waziri Jaffo aliupongeza uongozi wa shule hiyo na ule wa Wilaya ya Karagwe kwa ujumla kwa kutekeleza na kutunza miradi mbalimbali mara inapokamilika wilayani hapa.
Zaidi alioneshwa kuvutiwa na ujenzi wa maktaba unaoendelea katika shule ya msingi Ihembe, mradi ambao unafadhiliwa na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho ambapo Mh. Waziri Jaffo aliahidi kwa uongozi wa Wilaya ya Karagwe na kwa wananchi waliokuwa wamekusanyika kumsikiliza katika viwanja vya shule ya Msingi Ihembe ya kwamba ofisi yake inakusudia kuangalia namna ya kusaidia ujenzi wa maktaba hiyo pamoja na baadhi ya miradi ya shule za msingi na sekondari iliyoombwa kwa nyakati tofauti na mbunge wa Jimbo la Karagwe ambae pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Innocent Lugha Bashungwa.
Katika hatua nyingine Mh. Jaffo aliutembelea mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, uliopo eneo la Nyakanongo, mradi ambao umekamilika kwa zaidi ya asilimia 98, huku ukigharimu kiasi cha shilingi blioni moja na milioni mia nane ikiwa ni fedha kutoka serikali kuu na kiasi kingine cha shilingi 161, 477, 869.00 ikiwa ni fedha iliyochangiwa na Halmashauri ya Wilaya ambapo licha ya kupongeza jitihada za uongozi wa wilaya hii, Mh. Waziri Jaffo alitoa agizo kwa Halmashauri ya Wilaya kuendelea kutenga kutoka katika mapato ya ndani, fedha kwa ajili ya ukamilishwaji wa maeneo muhimu ambayo hayakamilika.
Aidha, katika hatua nyingine Mh. Waziri Jaffo, ameahidi kwamba ofisi yake itatoa kiasi cha shilingi bilioni moja ambapo kiasi cha shilingi milioni mia tano (500,000,000.00/=) itatumika kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wanaume na kiasi kingine kinachobaki kitatumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ili kukidhi mahitaji ya hospitali.
Ziara ya Mh. Jaffo, kwa mara nyingine ilitoa agizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, Mh. Godwin Kitonka na Timu ya Menejimenti kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato licha ya kupongeza hatua iliyofikiwa ya kukusanya mapato hayo zaidi ya asilimia 49 mpaka sasa.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.