WATUMISHI KARAGWE DC WAMSHUKURU DED KWA KUWEZESHA MAFUNZO YA AFYA YA AKILI.
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe wamemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bi.Happiness Msanga kwa kuwezesha Mafunzo ya Afya ya Akili kwa Watumishi ambayo yamewasaidia kuboresha afya zao za akili pamoja kuwapa uwezo kukabiliana na changamoto zao kwa utashi bila kuleta madhara.
Mafunzo haya yamefanyika kwa siku tano mfululizo kuanzia Septemba 14 hadi 18, 2025 kwenye Tarafa zote 5 za Wilaya ya Karagwe ambazo ni Bugene, Nyakakika, Nyaishozi, Kituntu na Nyabiyonza kuhakikisha Watumishi wote 2700 wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe wanapata Elimu hiyo iliyowasilishwa na Mkufunzi wa Afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt.Garvin Kweka.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti za Mafunzo, Watumishi hao wamemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karagwe Bi.Happiness Msanga kuhakikisha elimu hiyo inawafikia Watumishi wengi hadi waliopo vijiji vya mbali na makao makuu wanaamini elimu waliyopata itawasaidia kuweka usawa kwenye kazi na maisha yao (work & life balance).
Akizungumza kwa niaba ya Watumishi waliohudhuria mafunzo hayo katika Tarafa ya Bugene, Mtendaji wa kijiji cha Nyarugando Bw. Athanas Mapombe amesema mafunzo hayo yatamsaidia kujenga mahusiano mazuri kazini ikiwemo kusaidiana endapo ataona dalili za uwepo wa tatizo la afya ya akili kwa mtumishi mwenzie pia ameomba , kuwepo na semina kama hizo kila inapotokea fursa ili kujengeana uwezo zaidi katika mazingira ya kazi.
Naye, Mwalimu Grace Shibundulila wa shule ya msingi Bujara aliyehudhuria mafunzo hayo Tarafa ya Nyaishozi amesema mafunzo haya yatamsaidia kwenye kufanya maamuzi sahihi anapokua na msongo wa mawazo na kuweka usawa kwenye kutekeleza majukumu yake ya kazini na nyumbani.
Aidha, Mafunzo hayo yalitolewa pia kwa Vyombo vya Usalama Wilaya ya Karagwe, Wanafunzi wa Kidato cha Sita Shule ya Sekondari Bugene pamoja na Wananchi wa Wilaya ya Karagwe ambao Walikutana kwenye Ukumbi wa chuo cha VETA Wilayani humo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.