Na Innocent Mwalo.
Halmashauri ya Wilaya Karagwe imeendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 pamoja na agizo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia na Sheria ya fedha Na.4 ya mwaka 2018 inayozitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga asilimia 10 ya mapato ya ndani ikiwa ni mikopo yenye masharti nafuu na isiyo na riba kwa ajili ya mfuko wa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.
Hivi karibuni Halmashauri hii imetoa mikopo usiokuwa na riba wa jumla ya Tsh.88,000,000 kwa vikundi 31 ambavyo kati ya hivyo vikundi 24 ni vya wanawake na vikundi 7 vya vijana.
Awali katika taaarifa yake kwa mgeni rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hii, Mh. Geofrey Mheluka, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri hii Bi. Edina Kabyazi alimtaarifu mgeni rasmi huyo ya kwamba vikundi vilivyokuwa vinakabidhiwa mkopo ni vile ambavyo vimepewa Elimu juu ya kuhakikisha kwamba mkopo huu unatumika kwa malengo yaliyopangwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu na bila kutawaliwa na ubinafsi wala upendeleo.
”Napenda kusisitiza vikundi vyenye miradi mingine kuhakikisha fedha zote zinaingizwa katika shughuli za miradi na si vinginevyo, na taarifa ya mapato na matumizi ifahamike kwa wanakikundi wote’’, alisisitiza Bi. Edina.
Aidha pamoja na kuainisha changamoto ya baadhi ya vikundi kutorejesha mikopo kwa mjibu wa mkataba hasa vya vijana, Bi Edina aliahidi ya kwamba Idara yake itaendelea kufanya tathmini ya kina ili vikundi vinavyokidhi vigezo viweze kukopeshwa kiasi hicho kidogo.
Kwa upande wake Mh. Mheluka alitoa rai kwa wanavikundi kuwa waaminifu katika marejesho ili vikundi vingine pia vinufaike na fursa hii Huku akiagizwa kukabidhiwa kwake kwa orodha ya wale aliowaita wadaiwa sugu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bi. Edina kwa mgeni rasmi, Halmashauri ya wilaya ya Karagwe imeshachangia kiasi cha Tsh. 109,448.052 sawa na asilimia 10% ya mapato halisi yaliyokusanywa kwa kipindi cha tangu Julai 2020 hadi Disemba 2020. Aidha taarifa hiyo inaonesha ya kwamba tangu mwaka 2015/2016 mpaka sasa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe imeshachangia jumla ya Tsh 651,755,632/= kwenye mfuko wa wanawake,vijana na watu wenye ulemavu huku kiasi cha Tsh 1,331,488,000/= kikiwa kimekopeshwa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vipatavyo 526 vyenye wanufaika 9143.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.