WANAWAKE 187 WA JUMUIYA YA KIISLAM YA WILAYA YA KARAGWE WAPATIWA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI
Wanawake 187 wa Jumuiya ya Kiislam Wilaya ya Karagwe wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali ili kuwawezesha kuzalisha kwa faida na kunufaika fursa ya Mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri. Mafunzo haya yamefanyika Jumapili tarehe 17/11/2024 na yaliandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa ushirikiano na Idara ya Maendeleo ya Jamii pamoja na idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Bi. Happiness Msanga amesema kuwa Mafunzo hayo yanalenga kuwainua Wanawake kiuchumi kwa kuwajengea uwezo wa kutambua fursa za biashara zilizopo maeneo yao na kuzitumia ipasavyo katika kukuza mitaji yao sambamba na kuwaeleza namna ya kuongeza mitaji kupitia Mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwenye Halmashauri kwa ajili ya Vikundi vya Wanawake,Vijana na Watu wenye Ulemavu.
“Zamani wanawake tulizoea kuhudumiwa lakini kwa sasa mazingira yamebadilika hivyo tunawajibu wa kuanza kujishughulisha
Ili tusaidiane majukumu kwenye familia kwa kufanya hivyo hata matukio ya ukatili yanaweza kupungua kwasababu mengine yanatokana na utegemezi uliopitiliza na ukosefu wa fedha. Niwasihi kina mama wenzangu tutumie mafunzo haya kutambua fursa zilizopo na kuzitumia kujitengeneza ili tuweze kunufaika na mikopo ya Mama Samia ambayo inatolewa na Halmashauri” Alisema Bi.Happiness
Aidha, Bi. Happiness amewataka wanawake hao kuwa vinara wa kuhubiri amani na utulivu kipindi hiki ambacho tuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024. Pia amewasisitiza kuudhuria kampeni pindi zitakapoanza ili waweze kusikiliza sera na kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi utakaowapatia Viongozi watakaowaongoza ipasavyo.
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam Wilaya ya Karagwe Bi. Hidaya Kamuzora akizungumza kwa niaba ya Wanawake amemshukuru Mkurugenzi na Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa kutambua umuhimu wa elimu ya ujasiriamali kwao na kuwapatia mafunzo hayo ambayo yatawawezesha kuinuka kiuchumi na kuwafanya wawe na nidhamu ya pesa za biashara hali ambayo itawapunguzia utegemezi na kuleta maendeleo kwenye jamii.
Mafunzo yaliyotolewa kwa Wanawake hao ni maana halisi ya Ujasiriamali, Sifa za Mjasiriamali, Jinsi ya kutambua fursa za ujasiriamali, Namna ya kukuza mtaji na kuweka akiba, Mbinu za kibiashara pamoja na jinsi ya kutengeneza vikundi na namna ya kuomba mikopo ya Halmashauri.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.