WALENGWA WA TASAF KARAGWE DC WANUFAIKA NA VIKUNDI VYA HUDUMA NDOGO ZA KIFEDHA WALIZOANZISHA.
Walengwa wa Mfuko wa kusaidia kaya Masikini (TASAF) wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe wamenufaika na vikundi vya huduma ndogo za kifedha walizoanzisha kuanzia mwaka 2022 na 2023 kufuatia maelekezo ya Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti wakati walipotembelewa na Maafisa Wafuatialiaji, Waratibu na Wahasibu wa Mfuko wa TASAF Mkoa wa Kagera, Walengwa wa mfuko huo walieleza namna mbalimbali walivyofaidika na vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana walivyoanzisha ikiwemo kusomesha watoto shule, kuanza kufuga wanyama wadogo wadogo wakiwemo mbuzi, kuku, nguruwe pamoja na kurekebisha na kujenga makazi yao.
Aidha, Meneja Usimamizi na Ufuatiliaji kutoka Makao makuu ya TASAF Bi. Salome Mwakigomba amewapongeza walengwa hao kwa kuendelea kuvitumia vikundi hivyo kufanya maendeleo na kuwasisitiza kupendana wao kwa wao ili waweze kuinuana na kuchangiana kwenye biashara walizoanzisha.
Naye, Mratibu wa TASAF mkoa wa Kagera Bw. Efraz Mkama amesema kuwa Mkoa wa Kagera kwa mwaka 2024 ulipokea kiasi cha Billioni 118 na kuhudumia vijiji 728 ambapo kupitia fedha hizo Walengwa wameweza kutengeneza vikundi vya kununua hisa na kukopeshana, biashara ndogondogo, kununua vyakula pamoja na kununua sare za watoto za shule.
Kwa niaba ya vikundi vilivyoanzishwa, Kikundi cha upendo kilichoanzishwa mwaka 2022 kiliwasilisha taarifa ya kikundi hicho ambayo ilisomwa na Bw.Faustine Kushekwa ilieleza miradi inayofanywa na Walengwa ikiwemo kufuga wanyama wanyama wadogo, kuweka akiba na kukopeshana
Pia taarifa ilieleza kuwa Novemba kikundi hicho kitagawana faida.
Kwa upande wake Mnufaika wa vikundi hivyo ambae pia ni Mlengwa wa TASAF Bi. Adelphia Adolf ameushukuru mfuko wa TASAF kwa kuanzisha vikundi hivyo kwasababu vimewasaidia kuweka akiba ambazo wameweza kuzitumia kufanya maendeleo.
Hata hivyo kwa sasa, Mfuko wa TASAF kwa Wilaya ya Karagwe unahudumia Vijiji 84 na Kaya 9123.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.