WAJUMBE WA BARAZA LA WAFANYAKAZI LA HALMASHAURI YA WILAYA YA KAARAGWE WAASWA KUWA MABALOZI WAZURI WA KUFUATA KANUNI NA TARATIBU ZA UTUMISHI WA UMMA
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Wilaya Bi. Happiness J. Msanga amewaasa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kuwa mabalozi wazuri wa kufuata kanuni na taratibu katika utendaji kazi ikiwemo kutokujiusisha na makundi ya kisiasa hasa tunapoelekea kipindi cha uchaguzi mkuu 2025 ili kuwapa motisha Wafanyakazi wenzao waliowawakilisha katika kuleta chachu ya maendeleo Wilayani humo.
Bi.Happiness ametoa wito huo wakati wa kikao cha Bajeti cha Baraza la Wafanyakazi la Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kilichofanyika mapema leo tarehe 13/1/2024 katika Ukumbi wa Halmashauri (Angaza) na kuhudhuriwa na Wajumbe kutoka idara na vitengo vyote vya Halmashauri pamoja na Wawakilishi kutoka vyama vya wafanyakazi kama vile TUGHE,CHAKUHAWATA, CWT na TALGWU.
Akiwasilisha rasimu ya bajeti na mpango wa maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa mwaka 2025/2026 Ndg; Cyliacus Felician amesema kuwa Halmashauri imepanga kukusanya na kutumia jumla ya Sh. Bilioni 54,07 kwa mwaka huu wa fedha kwa matumizi mbalimbali ikiwemo ukamilishaji wa zahanati 8 zilizojengwa na wananchi na Uendelezaji wa miradi itakayoiongezea Halmashauri mapato.
Wajumbe walipata nafasi ya kuuliza na kutoa mapendekezo yao kufuatia rasimu ya bajeti iliyowasilishwa ambapo waligusia maswala ya namna ya kuwasaidia wanaoishi na virusi vya ukimwi kazini, ujenzi wa miundo mbinu ya maji kwenye vyoo vya shule ya msingi na sekondari, elimu jumuishi, Ushiriki wa watumishi kwenye michezo , madai ya likizo, kubadilishiwa miundo pamoja na malipo ya wafanyakazi waliohamishwa.
Aidha, Mwenyekiti wa kikao hicho Bi. Happiness Msanga alitoa majibu ya maswali yalioulizwa pamoja na kupokea mapendekezo yaliyowasilishwa kutoka kwa wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi na kuahidi kufanyia utekelezaji yanayotekelezeka kwa wakati.
Aidha, Bi.Happiness amewataka watumishi kuhakikisha wanajaza taarifa zao kwa usahihi ili kurahisisha zoezi la uhakiki wa taarifa pamoja na kuwahisha malipo. Pia ametumia nafasi hiyo kuwasisitiza Watumishi kushiriki mambo ya maendeleo ya kijamii kwenye sehemu wanazoishi ili kuongeza nguvu na morali ya wananchi katika ushiriki wao kwenye shughuli za maendeleo.
Hatahivyo, Bi Happiness amewasisitiza watumishi kuacha kutengeneza makundi ya kiutumishi ya kisiasa na kujihusisha na shughuli za siasa hasa tunapoelekea kipindi cha uchaguzi kwa mwaka huu 2025. Ameongeza kuwa, Watumishi wote wanapaswa kufuata miongozo na maelekezo ya ushiriki wa uchaguzi na si vinginevyo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.