WAJUMBE WA BARAZA LA MAMLAKA YA MJI MDOGO KAYANGA WAASWA KUSIMAMIA MATUMIZI SAHIHI YA BARABARA ZA MJI.
Mwenyekiti wa Baraza la Mamlaka ya mji mdogo Kayanga Mhe.Projest Kajuna ambaye pia ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Katoma Ruzinga amewaasa wajumbe wa baraza la mamlaka ya mji mdogo wa Kayanga kusimamia matumizi sahihi ya barabara za mji huo ili kuepukana na uharibu wa barabara hizo kutokana na matumizi ambayo si sahihi ikiwemo kupitishwa kwa magari yaliyozidi uzito pamoja na kushusha na kupakia mizigo kiholela.
Wito huo umetolewa na Mhe.Kajuna mapema leo Tarehe 27/01/2025 wakati wa kikao cha Baraza cha robo ya pili cha Mamlaka ya Mji mdogo Kayanga kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe (Angaza).
"Lazima tutunze barabara zetu kwasababu zimetengenezwa kwa gharama kubwa na zinatusaidia kwenye shughuli zetu. Niwasihi msimamie matumizi sahihi kwasababu maelekezo ya vituo vya kushusha na kupakia mizigo vipo na barabara zimejengwa kwa vipimo ambavyo inatupasa kuzingatia ili barabara zetu zidumu" alisema Mhe.Kajuna.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Bi.Happiness Msanga wakati akisalimia wajumbe wa Baraza hilo amewaomba wajumbe kutoa ushirikiano kwenye ukusanyaji wa mapato ambao kwa namna moja au nyingine wanahusika katika kubainisha vyanzo na ukusanyaji kwa maslahi mapana ya mji mdogo Kayanga na Halmashauri kwa ujumla.
Vilevile, Bi.Happiness ametumia nafasi hiyo kuwasihi wajumbe kutojihusisha kwenye migogoro ya ardhi ambayo imekua changamoto kubwa na endapo mauzo ya ardhi yatafanyika wajumbe wanapaswa kujiridhisha kwenye umiliki halali wa ardhi ili hata itapotokea ushahidi unahitajika uwe wa kweli pasipo na shaka.
Hatahivyo, Mhe.Kajuna alitoa wito kwa wajumbe kuhakikisha maeneo ya mji mdogo yanapimwa na kurasmishwa ili kuruhusu miradi ya serikali kuendelea bila malalamiko kutoka kwa wananchi mfano.Ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na TARURA.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.