Halmashauri ya wilaya ya Karagwe imeendelea kuneemesha vikundi vya wajasiriamali kwa kuwapatia mkopo wa shilingi 293,000,000. Mkopo huo umetolewa kwa vikundi 60 vya wanawake, vijana na walemavu kwa lengo la kuwasaidia wajasiriamali hao kukuza mitaji yao ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi mfano wa wa hudi kwa wanavikundi hao iliyofanyika kwenye ukumbi wa Angaza Julai 1, 2022. Mkuu wa wilaya ya Karagwe, Mhe. Mwl.Julieth Binyura amewataka wanavikundi kutumia mkopo waliopewa kwa weledi na maarifa ya kutosha.
“Ili mkopo uwe na tija kwenye familia zenu, ni lazima muangalie shughuli mnazozifanya na kutafakari kama shughuli hizo zina faida kiuchumi au la, ili muweze kutafuta shughuli mbadala”. Alisema Mhe. Binyura.
Mhe. Binyura ameendelea kusisitiza kwamba wakati tukielekea kwenye biashara za kitaifa na Kimataifa, wajasiriamali hao wajipange kwa ajili ya kupata wateja wa kigeni kwani tupo mpakani mwa nchi za Uganda na Rwanda.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Karagwe , Michael Nzyungu amewakumbusha wajasiriamali hao kutambua kuwa fedha hizo wamekopeshwa na wanatakiwa kuzirejesha na kubakia na faida . Kumekuwa na baadhi ya wanakikundi wanaokopa fedha za kufanyia biashara lakini wanazitumia kinyume na malengo ya mikopo hiyo.
Awali akisoma taarifa ya mikopo, Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii, Bi. Edina Kabyazi amesema kuwa , kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni 2022, Halmashauri imetowa mkopo wa kiasi cha shilingi 293,000,000 kwa vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu vipatavyo 60. Ufuatiliaji wa mikopo unaendelea na kwa mwezi aprili hadi juni 2022, jumla ya shilingi 111,448,650 zimerejeshwa. Pamoja na marejesho hayo, kiasi cha shilingi 789,052,846 bado zinadaiwa na kati ya hizo, shilingi 267,750280 ni deni la nje ya mkataba wa utaratibu wa mikopo wa sasa.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.