UFAULU WA ASILIMIA 100 WAWAPELEKA WALIMU WA KIDATO CHA TANO NA SITA HIFADHI YA TAIFA YA NGORONGORO.
Agosti 8, 2025 Walimu wa kidato cha tano na sita wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe walipata nafasi ya kutembelea eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ikiwa ni motisha baada ya matokeo mazuri ya kidato cha sita 2025 ambapo kwa shule zote 5 za Wilaya ya Karagwe zilifaulisha kwa asilimia 100.
Matokeo yalikua kama ifuatavyo Daraja la kwanza Wanafunzi 272, Daraja la pili 130 na Daraja tatu 10 Hakuna Daraja la nne wala sifuri kwenye shule zote tano (Nyabionza, Bugene, Kituntu,Karagwe na Nyaishozi).
Akizungumza wakati wa mahojiano na kitengo cha mawasiliano Serikalini Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe: Julius Kalanga Laizer amesema kuwa Serikali inatambua juhudi za walimu katika ufaulu wa wanafunzi na Wilaya itaendelea kuwatia moyo na kuwaunga mkono kwa kuwapa motisha mbalimbali ili kuongeza ufaulu zaidi kwenye madarasa ya mitihani.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Bi; Happiness J. Msanga amesema kuwa Motisha ni moja ya kanuni ya Utumishi wa umma Kwa kutambua mchango wa walimu katika ufaulu wa wanafunzi Halmashauri iliandaa ziara ya walimu kwenye hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ili wakajifunze mambo mbalimbali ya kihistoria pamoja na kuwaongezea ari ya kufundisha ili kuongeza ufaulu kwa Wanafunzi.
"Ni ukweli usiopingika hakuna Mwanafunzi anayeweza kufaulu bila jitihada za walimu hata mimi nisingekuwa hapa nilipo bila ya walimu, tunatambua na kuwathamini walimu. Ziara hii ni motisha baada ya matokeo mazuri na ikawafanye wafanye vizuri zaidi matokeo ya mwakani kwasababu huu ni mwanzo tu, kuna mazuri zaidi" Alisisitiza Bi. Happiness
Aidha, kwa nyakati tofauti tofauti za mahojiano baina ya kitengo cha mawasiliano serikalini Walimu wamefurahishwa na ziara hiyo na wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa ubunifu, ufanisi na kwa juhudi zaidi ili wafikie ufaulu wa asilimia zaidi ya 100 kwa kuongeza daraja la kwanza, la pili na kuondoa daraja la tatu, nne na sifuri. Pia, wametoa shukrani zao za dhati kwa Serikali kwa uwekezaji kwenye sekta ya elimu pamoja Mkurugenzi Mtendaji kwa kutambua juhudi zao.
Vilevile, Bi. Happiness amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan chini ya Serikali ya awamu ya sita kwa usimamizi mzuri wa sekta ya elimu pamoja uwekezaji mkubwa uliofanyika ikiwemo kuongeza shule za kidato cha tano na sita Wilaya ya Karagwe ambapo awali kulikuwa na shule 5 tu na sasa zipo 8 zinazotarajia kufanya mitihani mwakani 2026.
Hatahivyo, Motisha kwa Watumishi ni muhimu kwasababu inachochea ubunifu, kupunguza migogoro pamoja na kuongeza uwajibikaji.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.