Na Innocent E. Mwalo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, ndugu Godwin Kitonka, kwa mara nyingine, amewaagiza watendaji wa vijiji na kata wilayani hapa kulifanya suala la lishe kuwa ni moja ya vipeumbele katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kuwaonya wale watakaolega katika kutekeleza agizo hilo la serikali ya kwamba serikali haitasita kuchukua hatua dhidi yao kwa mujibu wa sheria.
Ndugu Kitonka alitoa maelekezo haya kwa watendaji wa kata wilayani hapa katika kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe kilichofanyika katika ukumbi Angaza ambayo kikao hicho kiliwahusisha watendaji hao wa kata na baadhi ya wataalam kutoka katika Idara mbalimbali za Halmashauri ya wilaya.
‘’Naomba kuwaeleza kupitia kikao hiki kuwa suala la lishe katika vijiji na kata zenu sio la hiari tena, ninyi watendaji wa kata nendeni mkavisimamie kata zenu na vijiji vilivyopo katika maeneo yenu, ili kwa mwezi mmoja toka tarehe ya kikao hiki, kila kijiji na kata kikafufue au kuunda upya (kama hamna) kamati za lishe kwenye ngazi hizo za kata na vijiji’’, alisema Kitonka.
Kitonka alisisitiza,’’ Lakini sio tu mkafufue nakuunda kamati hizo, bali nendeni mkahakikishe orodha ya wajumbe wa kamati hizo za lishe zinabandikwa kwenye mbazo za matangazo kwa kila kijijii na kata ili wananchi kwenye maeneo hayo wapate kuwatambua wajumbe hao’’.
Ndugu Kitonka alienda mbali na kuwaagiza watendaji wa kata kuhakikisha katika kila kata na vijiji kunakuwa na majalada yenye mihtasari ya vikao vya lishe na katika mikutano mikuu ya vijiji pamoja na ile ya kamati za maendeleo ya kata (KAMAKA) agenda ya lishe iwe ni suala la kudumu.
‘’Kwa kuwa suala la utapiamlo ni kubwa sana katika mkoa wa Kagera, kwa mara nyingine natoa maagizo kwa watendaji wa vijiji na kata pamoja na wale watumishi wanaohusika na huduma ya afya ya kwamba ili suala la udumavu liweze kukomeshwa wilayani hapa, hatuna budi kufanya pia ufuatiliaji kwa akina mama wajawazito ili kurekebisha kasoro hizo kabla ya watoto kuzaliwa’’, alisema ndugu Kitonka.
Katika hatua nyingine ndugu Kitonka aliwaeleza washiriki wa kikao hicho juu ya dhamira ya serikali katika Halmashauri ya wilaya hii katika kulithamini suala la lishe ambapo kwa kuanzia kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Halmashuri ya wilaya imetenga bajeti ya kiasi cha shilingi milioni 83 kwa ajili ya kutekeleza shughuli zinazohusiana na masuala ya lishe.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.