Na Innocent E. Mwalo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Godwin Kitonka ametoa maelekezo kwa wataalam wa ngazi za msingi, sekta za Afya, Elimu, Kilimo, Mifumo, Uvuvi na fedha pamoja na Kamati yote ya lishe kuhakikisha yale yanayoazimiwa kwenye vikao na mkataba wa lishe yanatelezwa ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) alisainiana na Wakuu wa Mikoa na kisha Wakuu wa Mikoa wakasainiana na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Wilaya wakasainiana na Wakurugenzi Watendaji wa Wilaya.
Mh. Kitonka aliyasema haya kwenye kikao cha Kamati ya Lishe wilaya kwa robo ya nne na ya mwisho kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo pamoja na mambo mengine kilipokea taarifa na mikakati mbalimbali ya Idara za serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo katika ajenda ya kupambana na tatizo la utapiamulo ambapo takwimu zinaoonesha kuwa mkoa wa Kagera tatizo la utapiamulo ni kwa zaidi ya asilimia 33.
‘’Baada ya kikao hiki ningependa kuona kamati hii na wadau wote wa lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kuhakikisha kuwa wanatembelea maeneo yenye shida ya lishe ili kutoa elimu katika jamii kwani kwa imani yangu wilaya yetu ya Karagwe haina tatizo kabisa na suala la upatikanaji wa makundi yote ya vyakula yanayotajwa kufanya mlo kamili ila tatizo ninaloliona mimi ni juu ya uelewa wa wananachi wetu katika kula vyakula vyote vya makundi haya iliwemo wanga, protini, vitamin na kadhalika’’, alisisitiza Kitonka.
Maazimio mengine yaliyotolewa katika kikao hicho ilikuwa ni pamoja na wakuu wa shule na walimu wakuu kuhakikisha kuwa wanakuwa na maeneo katika shule zao yanajishughulisha na kilimo ili kuwezesha wanafunzi kupata chakula cha mchana na matunda wawapo shuleni.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.