Na Innocent E. Mwalo.
Harambee iliyoandaliwa na wananchi wa kata ya Bugene chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata ambaye pia ni diwani wa kata hiyo, Mh. Mugisha Anselim Mathias imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi 42,782,750,000/= zitakazotumia katika ujenzi wa shule ya sekondari na zahanati katika kata hiyo.
Katika harambee hiyo mgeni rasmi, mbunge wa jimbo la Karagwe ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mhe. Innocent Lugha Bashungwa, alimmiminia sifa kemkem Mh. Mugisha kwa kuona mbali na kuja na wazo hilo la kuanzisha ujenzi wa shule ya sekondari pamoja na zahanati katika eneo hilo la kata ya Bugene kutokana na ukweli kwamba licha ya makao makuu ya wilaya ya Karagwe kuwa katika kata ya Kayanga lakini kata ya Bugene inabaki kuwa ni moja kati ya kata ambazo zinaongoza kwa kuwa na ongezeko kubwa la watu hali inayopelekea uhitaji wa huduma hizo muhimu za shule ya sekondari na zahanati kwa sasa na kwa kipindi kijacho.
Mh. Bashungwa, huku akirejea baadhi ya takwimu zilizotolewa kupitia taarifa ya Mh. Mugisha ambayo ilionesha kwamba kutokana na kata ya Bugene kuwa na shule moja tu ya sekondari mathalani kwa mwaka huu 2021 kidato cha kwanza katika shule ya Bugene kina idadi ya wanafunzi wasiopungua 300 hali inayotajwa kwamba isipokabiliwa kwa jitihada kubwa ya kujenga shule nyingine mpya ya sekondari kwa sasa huenda ikaathiri utoaji wa elimu katika kata hiyo kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
‘’Naomba madiwani wote wa kata nyingine 22 zilizopo katika wilaya ya Karagwe tuyaone maono haya Mh. Mugisha kama changamoto kwetu iltakayotuwezesha kufikiria juu ya namna ya kuanzisha miradi kama hii kwenye kata zetu’’, alisema Mh. Bashungwa.
Harambe hiyo iliyoendeshwa kwa ustadi mkubwa na Padre Sixmund Nyabenda, ambaye ni padre wa kanisa katoliki, jimbo katoliki la Rulenge -Ngara ilihudhuriwa na wageni wengine mashughuli akiwemo mkuu wa wilaya ya Karagwe, Mh. Julieth Binyura ambaye aliambatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi ya wilaya, Mwenyekiriti wa Halmashauri ya wilaya, Mh. Wallace Mashanda aliyekuwa ameambatana na baadhi ya madiwani akiwemo mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji Mh. Charles Beichumila. Aidha, wageni wengine waaalikwa walikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ndugu Godwin Kitonka na baadhi ya wataaalum kutoka katika timu ya menejimenti ya wilaya.
Katika kiasi cha shilingi cha Shilingi 42,782,750,000/= ambacho kilichangwa, shilingi 12,6750,000/= zilitolewa kama fedha taslimu na kiasi kiasi kinachobaki kilitolewa kama ahadi huku michango mingine kama vile viwanja vyenye ukubwa wa ekari 7, matofali 1000, mti mmoja, gunia moja maharage, ng’ombe mmoja na michango mingine ya msaada wa kuezeka kwa paa la majengo hayo pale jengo hilo litakapofikia hatua hiyo ya kuezekwa, msaada ulioahidiwa na benki ya NMB Karagwe iliahidiwa pia kupitia harambee hiyo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.