Mwenyekiti wa halmashauri ya karagwe na diwani wa kata ya Nyaishozi Mhe: Wallace Mashanda amewatangazia kiama watu wote wanaoharibia wanafunzi masomo pamoja na kuua ndoto zao za kusoma.
Ameyasema hayo wakati wa mahafali ya 15 ya kidato cha nne ya shule ya sekondari Kawela na ukaribisho wa kidato cha tano kwa wanafunzi wa kike iliyofanyika Agosti 28 ,2024 katika viwanja vya shule hiyo.
“Niwaonye wote wenye tabia ya kuwaharibia wanafunzi masomo yao kwasababu hatutakuwa na huruma kwenye hilo. Wazazi wanawekeza pesa nyingi kusomesha, Serikali pia imewekeza na kuipa elimu kipaumbele. Tumeshuhudia shule mpya na miundo mbinu wezeshi naomba tuitumie vizuri kuhakikisha watoto wetu wanasoma mpaka elimu za juu”
Aidha, Mhe: Mashanda amewasisitiza wazazi kuwaendeleza watoto waliomaliza kidato cha nne kwenda kidato cha tano au vyuo vya ufundi badala ya kuwaacha nyumbani pia amewataka wazazi kushirikiana na uongozi wa shule kukomesha utoro shuleni ambao umekua changamoto.
Hata hivyo, Mhe: Mashanda amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Jimbo la Karagwe Mhe: Innocent Bashungwa kwa kuipatia shule ya Kawela zaidi ya sh Million 582 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule ili kuwapa wanafunzi mazingira bora ya kujisomea na kufikia ndoto zao.
Pia Mkuu wa Shule wa Sekondari Kawela Ndg: Joel Kamanda ameishukuru Serikali kwa kuipatia shule mradi wa Maji, Fedha za Madarasa na matundu ya vyoo. Pia ameishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa kuipatia shule sh Million 12 kwa ajili ya ujenzi wa bwalo.
Vile vile, Shule ya kawela imepokea wanafunzi wa kidato cha tano kwa mara ya kwanza kutoka Mikoa mbalimbali nchini kwa michepuo ya sayansi na sanaa.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.