Na, Geofrey A. Kazaula
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brig, Jen Marco E. Gaguti ameupokea mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa pamoja na Ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi Chema iliyopo Kata ya Nyakabanga Wilayani Karagwe
Mradi huo umekamilika baada ya kuwa umejengwa na Shirika lisilo la kiserikali la Jambo Bukoba kwa shirika hilo kuchangia 60% ya ujenzi ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ilichangia 30% ya ujenzi huo na nguvu za wananchi ni asilimia 10% ambapo thamani ya mradi huo ni T.Sh 66,000,000.00.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza wakati wa kukabidhiwa kwa mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera amesisitiza juu ya utunzaji wa mradi huo ili kufikia malengo ya Serikali ya kutoa elimu kwa wanafunzi.
Amesisitiza kuwa jamii iendelee na moyo wa kujitoa katika kuchangia miradi yao na kwamba Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali wa maendeleo katika Mkoa wa Kagera ili kukamilisha miradi inayokuwa imechangiwa na wananchi.
‘‘ Mradi huu ni mzuri sana hivyo jamii pamoja na walimu kuna wajibu mkubwa wa kuutunza mradi huu ili ufanye kazi zilizokusudiwa, lengo la mradi huu ni kutumika sasa, kesho na siku za badae ili kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu bora hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu hapa kuhakikisha mradi huu unatunzwa’’. Alisema kiongozi huyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Ndg, Jackson Mwakisu amefafanua kuwa Halmashauri inao mpango wa kuendelea kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia mapato yake ya ndani na kuwataka Shirika la Jambo Bukoba kutambua kuwa Halmashauri haitasita kuchangia pale Shirika hilo litakapo jitokeza tena kusaidia katika miradi mingine.
‘‘ Nitumie fursa hii kuwapongeza Shirika la Jambo Bukoba pamoja na wananchi waliochangia mradi huu, sisi kama Halmashauri kupitia mapato yetu ya ndani tutaendelea kuchangia katika kukamilisha miradi mbalimbali inayofadhiliwa na wadau na hivyo na waalika tena kuchangia hata maeneo mengine kwani mahitaji hasa ya miundombinu bado ni makubwa’’. Alisema iongozi huyo.
Maradi huo pia ulihusisha utengenezaji wa madawati kwa kila darasa pamoja na kiti kimoja cha mwalimu.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.