Na Innocent E. Mwalo.
Katika kutekeleza agizo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Sheria ya Fedha namba 4 iliyotungwa na Bunge hilo mwaka 2018 ambayo inayozitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani ya kila mwezi kwa ajili ya mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa kipindi cha Januari – Machi, 2021 imetenga na kutoa kiasi cha shilingi 138,000,000/= ikiwa ni mkopo kwa vikundi 42 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Hafla ya makabidhiano ya fedha hizo ilifanyika katika Ukumbi wa Vijana Rafiki wa Angaza, mnamo Aprili 18, 2021, ambapo viongozi waandamizi wa Halmashauri na Wilaya akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mh. Godfrey Mheluka, Katibu Tawala Wilaya, Mh. Innocent Nsena, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Mh. Wallace Mashanda na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ndugu Godwin Kitonka, kwa nyakati tofauti walitoa maelekezo muhimu kwa wanavikundi hao waliopokea mkopo huo.
Mh. Mheluka pamoja na mambo mengine, aliwahimiza na kuwaagiza wanufaika wa mkopo huo kuhakikisha mkopo huo walioupata unatumika kwa malengo yaliyopangwa na kukusudiwa ambapo kila kikundi kiliaswa kuzingatia kanuni na taratibu walizojiwekea bila kutawaliawa na ubinafsi.
‘’Kumewekuwa na changamoto mbalimbali za urejeshaji wa mikopo hii hasa kwa kundi la vijana licha ya kwamba mikopo hii inatolewa bila riba yeyote lakini baadhi ya vijana wanaonekana kutokuwa waaminifu, hivyo mitumie hafla hii kuwaagiza ninyi mnaopewa mkopo huu leo kuhakikisha marejesho ya mkopo huu yanafanyika kila mwezi kwa mujibu wa mkataba wenu kwani kipindi cha miezi mitatu mnachopewa kama kipindi cha neema kinatosha sana kujipanga kwa ajili ya kuanza kufanya marejesho ya mikopo hii kuanzia Agosti 2021, na mtapaswa kumaliza marejesho hayo mwezi Aprili, 2022’’, alisisitiza Mh. Mheluka.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Mh. Kitonka, alitoa wito kwa kundi la watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya kuomba mikopo hiyo ambapo aliwaambia watu wenye ulemavu ya kwamba serikali imelegeza masharti ya ukopaji kwa kundi hilo ambapo kwa sasa hata mtu mmoja anaweza kuomba mkopo huo pale anapokosa watu wa kuunda nao kundi hilo kwa ajili ya kupata mkopo hiyo.
Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Edina Kabyazi aliviagiza vikundi hivyo kuhakikisha kuwa vinawasilisha taarifa ya maendeleo ya kikundi inayoonyesha mafanikio na changamoto za kikundi.
Kwa upande mwingine chombo hiki lilitembela na kuangazia miradi mbalimbali iliyokwisha kupewa mikopo na Halmashauri ya Wilaya hii kwa vipindi tofauti na mradi mmojawapo uliotembelewa ulikuwa ni ‘Yes Group’ uliopo eneo la Kayanga ambao mwaka 2020 ulipewa mkopo wa kiasi cha shilingi milioni saba na ukafanikiwa kujenga kiwanda cha kuchakata alizeti kwa ajili ya kutengeneza mafuta ya kupikia.
Tangu mwaka 2015/2016 mpaka hivi leo, Halmashauri ya Wilaya imechangia kiasi cha Tshs. 715,244,385/= kwenye mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu huku kiasi cha Tshs. 1,466,488,000/= kikiwa kimekopeshwa kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu vipatavyo 570 na wanufaika 9,643.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.