Na Innocent E. Mwalo.
Kupitia mkutano maalum wa Baraza la Madiwani uliofanyika tarehe 24/06/2021, katika Ukumbi wa Angaza, mgeni rasmi katika mkutano huo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mh. Meja Jenerali, Charles Mbuge, ametoa maagizo mazito kwa uongozi na menejimenti ya Halmashauri ya wilaya ya Karagwe.
Kupitia mkutano huo uliokuwa maalum kwa ajili ya kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Mkuu wa Mkoa, Mh. Meja Jenerali Mbuge, aliuagiza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Karagwe kuweka uwazi katika utendaji kazi, kukusanya mapato ya Halmashauri ya wilaya kwa nguvu zote na kufanya kazi kwa uaminifu na weledi mkubwa.
Maagizo mengine ya mkuu wa mkoa yalikuwa ni juu ya suala la ubunifu kwa ajili ya kuleta maendeleo, ushirikiano miongoni mwao, kutoogopa watendaji walio chini ya menejimenti na kuwa macho na suala wahamiaji haramu ambalo ni tatizo la mara kwa mara linaloukumba mkoa wa Kagera na Wilaya ya Karagwe kwa ujumla.
Maagizo haya ya Mkuu wa Mkoa, hasa lile la kuweka uwazi katika utendaji wa kazi na kutoogopa watendaji walio chini yao yalitokana na mchango uliibuliwa na madiwani kadhaa ambao ni wajumbe wa mkutano huo akiwemo Mh. Dawson Byamanyirwohi diwani kutoka Kata ya Rugera, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmasahuri ya wilaya, ambaye katika michango yake aliyoitoa mara kadhaa katika majadiliano ya hoja hiyo aliwaomba madiwani wenzie waridhie kusudio lake la kumuomba mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali awe anaweka orodha ya majina ya watumishi wanasababisha kutokea kwa hoja.
‘’Naomba kuwaambia kuwa nitakuwa mkali wale watakaokiuka au kushindwa kuteleza maagizo ya CAG [Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali]’’, alisisitiza Mh. Meja Jenerali Mbuge.
Ushauri huo wa Mh. Byamanyirwohi na baadhi ya madiwani wengine waliochangia hoja hiyo ulikuwa ni kuunga mkono baadhi ya maagizo aliyotoa mkuu wa mkoa wa katikahotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo ambapo pamoja na mambo mengine, Mh. Mkuu wa Mkoa aliagiza kuchukuliwa hatua kwa wale wote waliotajwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kuwa walisababisha hasara na upotevu wa fedha kwani ripoti hiyo inaonesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Halmashauri ya wilaya ya Karagwe ilipata hati yenye mashaka huku ikiwa na hoja 57; hoja 33 zikiwa ni mpya, 24 zikiwa ni hoja za nyuma na maagizo manne (04) yakiwa ni maagizo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge (LAAC).
Kwa kuwa katika hoja nyingi mpya na zile za zamani changamoto kubwa iliyojitokeza katika ukaguzi ilikuwa ni malipo yaliyofanyika bila kuwa na viambatanisho au malipo yaliyofanywa bila kuwa na stakabadhi ya kukiri mapokezi, Mh. Meja Jenerali, Mbuge aalitoa melekezo kwamba kwa kuwa suala la ufuatiliaji na kukosekana kwa baadhi ya nyaraka muhimu linaloonekana kuwa ndio kiini cha hoja nyingi kuendelea kuwepo, hivyo alitoa muda wa siku saba (07), yaani juma moja, kutoka tarehe ya mkutano huo, kwa menejimenti kuhakikisha vielelezo vyote vitakavyosaidia kufutwa kwa baadhi ya hoja vinapatikana.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mh. Julieti Binyula, ambaye pia alitumia mkutano huu kujitambulisha kwani ilikuwa ni mara ya kwanza kuhudhuria mkutano kama huo toka alivyoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan, alitumuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa licha ya ugeni wake katika wilaya hii ila alibahatika kulisoma kabrasha la mkutano huo hivyo alibaini baadhi ya masuala yaliyosababisha Halmashauri ya wilaya hii kupata hati yenye mashaka na aliahidi kwa mkuu wa mkoa kuwa atafanya kazi na Halmashauri ili kuhakikisha kutokujirudia kwa hali hiyo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.