KUELEKEA MSIMU WA KAHAWA 2025/2026: MAAFISA UGANI KARAGWE DC WAPEWA MAFUNZO ILI KUWASAIDIA WANANCHI KUONGEZA THAMANI YA ZAO HILO.
Kuelekea msimu wa zao la Kahawa kwa mwaka 2025/2026 katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Maafisa ugani wa kata zote 23 wamepewa mafunzo rejea ili waweze kuwasaidia wananchi kuzalisha kahawa bora pamoja na kuongeza thamani ya zao hilo.
Mafunzo hayo yamefanyika mapema leo Tarehe April 11, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri (Angaza) yakiwa na lengo la kukumbushana wajibu wa Maafisa ugani katika kuhakikisha wananchi wanazalisha kahawa bora, kuongeza uzalishaji, pamoja na utoaji wa vibali vya kusafirisha na kuuza zao hilo.
Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Ndg. Augustino Lawi amesema kuwa kila Afisa Ugani anawajibu wa kuhakikisha Wakulima wanapata chakula bora na kuwatajirisha kwa kuwaelekeza namna ya kuongeza thamani mazao wanayozalisha pamoja na kuiongezea Halmashauri mapato.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Eng. Petro Mchele amesema kuwa Mafunzo hayo yatasaidia kuhakikisha zao la kahawa linakuwa endelevu na lenye tija katika kuongeza mapato kwa Wananchi na Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa zao la Kahawa Wilaya ya Karagwe Ndg. Paul Magorima ameongeza kuwa, kupitia mafunzo hayo maafisa ugani wataweza kuwasaidia wananchi kutambua ni aina gani ya kahawa inakubalika sokoni kwa kuzingatia ubora ambao unahusisha ukomavu wa kahawa, kiwango cha unyevu unyevu pamoja na utunzwaji wa zao hilo kabla ya kupelekwa sokoni.
Aidha, Maafisa Ugani walioudhuria mafunzo hayo wameishukuru Ofisi ya Mkurugenzi pamoja na Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kuandaa mafunzo hayo ya zao la kahawa na kuomba kupata nafasi ya kupewa mafunzo ya mazao mengine ili waweze kubadilishana na kuongezeana ujuzi ili kukuza uchumi wa Wananchi wa Wilaya ya Karagwe, Halmashauri na Taifa kwa ujumla.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.