KUELEKEA KILELE CHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI MACHI 08, 2025.
Kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani tarehe 08, Machi 2025, Wanawake wa kijiji cha Bujara wamejitokeza kushiriki zoezi la kuchota maji kwa ajili ya matumizi katika ujenzi wa zahanati ya kijiji. Zoezi hilo limeongozwa na Idara ya Maendeleo ya jamii kwa ushirikiano na Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wa kijiji hicho, lengo likiwa ni kuhamasisha Wanawake kushiriki kwenye shughuli za Maendeleo katika Jamii.
Zoezi hilo limefanyika mapema leo tarehe 25/03/2025 kwenye eneo la Zahanati ya Kijiji cha Bujara, Kata ya Nyakasimbi katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Akiongoza zoezi hilo, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Nyabionza Mhe. Jovitha Kombe amewapongeza Wanawake hao kwa kujitoa kwa hali na mali katika kufanikisha ujenzi wa Zahanati hiyo ambayo itakua msaada mkubwa kwa Wananchi wa kijiji cha Bujara. Pia amewataka Wanawake kuendelea kuhamasishana kushiriki shughuli za maendeleo na kutokubaki nyuma.
Naye, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi. Henrietta William amesema kuwa, Kuelekea Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe imejipanga kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuamsha ari ya ushiriki wa Wanawake katika miradi ya Maendeleo. Pamoja na kutoa kwa jamii kwa kuwezesha Wanawake na Wasichana waliopo kwenye mazingira magumu ili maadhimisho hayo yawe na tija kwa Wanawake na Jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake,Diwani wa Kata ya Nyakasimbi mhe.Vallence Kasumuni ameishukuru Serikali kwa kuungamkono juhudi za Wananchi katika ujenzi wa Zahanati hiyo. Ameongeza kuwa, Zahanati hiyo tayari imeshapokea kiasi cha shillingi Mil 28 kutoka Halmashauri na Mfuko wa Jimbo ili kuongeza nguvu kwenye ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Bujara.
Zoezi hilo liliambatana na utoaji elimu wa fursa zinazopatikana kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa Wanawake ikiwemo Mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu pamoja na Elimu ya Ujasiriamali. Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Wanawake kwa Wilaya ya Karagwe yatafanyika katika Kata ya Ndama kijiji cha Kagutu.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.