Na Geofrey A. Kazaula
Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe imeendelea kutekeleza maagizo ya Serikali kwa kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwaajili ya kutoa mikopo kwa wanawake, Vijana na wenye ulemavu.
Akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa kutoa mikopo kwa Robo ya tatu 2018/2019, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Ndg, Godwin M.Kitonka ame eleza kuwa Halmashauri kupitia Idara ya maendeleo ya Jamii itaendelea kutoa elimu kwa Vijana ili wajitambue zaidi na waone fursa ya kutumia mitaji kidogo kujiletea maendeleo.
Amefafanua kuwa Vijana wanapaswa kuelekezwa namna ya kuunganisha nguvu zao kuanzisha viwanda vidogo vidogo ili kujiongezea kipato na kwamba Halmashauri itaendelea kutoa mikopo hasa kwa vikundi vinavyofanya vizuri na kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
‘‘ Nitoe wito kwa wakopeshwaji hasa vijana , kuna haja sasa ya kujitahidi kukuza mitaji yenu na sisi kama Serikali tutaendelea kuwakopesha ili mfikie hatua ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo na suala hili lina wezekana kama watu watabadilika na kuona fursa hasa vijana wetu’’ alisema kiongozi huyo.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mh, Wallace Mashanda amefafanua kuwa vikundi vya wanawake vinaonekana kufanya vizuri katika kurejesha mikopo ukilinganisha na vikundi vya Vijana na hivyo amewataka vijana kubadilika na kuwa waaminifu ili kurejesha fedha kwa wakati na kuwezesha wengine kukopeshwa.
‘‘ Vikundi vingi vya Vijana vimekuwa havifanyi vizuri katika kurejesha mikopo ukilinganisha na Vikundi vya akina mama , natoa wito kwa vijana kubadilika na kuona kuwa fedha hizi tunazotoa zinatakiwa zirejeshwe kwa wakati ili tuwakopeshe na wengine’’ alisema kiongozi huyo.
Jumla ya T.Sh 80,000,000.00 zimetolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye Ulemavu katika Robo ya tatu ya mwaka 2018/2019 ambao jumla ya vikundi 37 vimepatiwa mikopo isiyo na riba.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.