KARAGWE DC YAJIPANGA KUUWAKILISHA MKOA WA KAGERA KWENYE MASHINDANO YA UMITASHUMTA NGAZI YA TAIFA.
Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha inauwakilisha mkoa wa Kagera kwenye Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) ngazi ya Taifa yanayotarajiwa kufanyika mkoa wa Iringa kuanzia Juni 07, 2025 hadi Juni 18,2025.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo ngazi ya Wilaya yaliyofanyika jana tarahe 22/05/2025 katika Uwanja wa Michezo wa Bashungwa, Afisa Michezo wa Wilaya ya Karagwe ndg. George Sebastian amesema Wanafunzi wamefanya maandalizi ya kutosha na ana imani kubwa Wilaya ya Karagwe itauwakilisha Mkoa wa Kagera.
" Kuanzia Mei 26 hadi 29,2025 Wilaya yetu itashiriki mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa yatakayofanyika Wilaya ya Muleba, Chuo cha Uwalimu Katoke. Niwahakikishie tutashinda vikombe vingi na matarajio yetu ni kuuwakilisha mkoa wa Kagera ngazi ya Taifa" Alisisitiza ndg Sebastian.
Sambamba na hilo, ndg. Sebastian ameongeza kuwa mwaka 2024 Timu ya mpira wa wavu ya Wilaya ya Karagwe ilifanikiwa kuuwakilisha Mkoa wa Kagera kwenye Mashindano hayo ngazi ya Taifa kwahivyo hana shaka na maandalizi ya mwaka huu katika kuhakikisha karibu timu zote zinazoshiriki kwenye ngazi ya mkoa kupata nafasi ya kwenda ngazi ya Taifa.
Aidha, Michezo itakayoshindanishwa ngazi ya Mkoa na Taifa itahusisha Mpira wa miguu kwa Wasichana na Wavulana, Mpira wa wavu kwa Wavulana, Mpira wa Netiboli, Mpira wa Mikono kwa Wavulana, Riadha kwa Wavulana na Wasichana, Kwaya, Ngoma na Mziki wa Kizazi kipya.
Hatahivyo, Mashindano ya UMITASHUMTA kwa mwaka 2025 yamebeba kauli mbiu isemayo " Viongozi Bora ni Msingi wa Maendeleo ya Taaluma, Sanaa na Michezo. Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Amani na Utulivu".
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.