KARAGWE DC YAFANYA KIKAO CHA AWALI KUANDAA BAJETI YA UTEKELEZAJI WA HUDUMA ZA LISHE 2025/2026
Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kupitia Idara ya Afya kwa kushirikiana na Sekta mtambuka pamoja na Wadau mbalimbali imefanya kikao cha awali kuandaa mpango bajeti wa utekelezaji wa awali wa huduma za lishe kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Bi. Beatrice Laurent ambaye pia ni Afisa Afya wa Wilaya amesema kuwa bajeti ya utekelezaji wa huduma ya lishe kwa mwaka 2025/2026 itafuata muongozo uliotolewa na Serikali katika kuhakikisha jamii inataarifa sahihi kuhusiana na ulaji wa vyakula vyenye virutubisho ili kuepukana na udumavu.
“Tumefanya kikao cha awali cha kuandaa bajeti itakayotuongoza kutekeleza huduma za lishe kwa mwaka 2025/2026 kwa kuzingatia muongozo unavyotutaka na changamoto tunazopitia kama Mkoa na Wilaya kuhusiana na Lishe. Makadirio ya bajeti hii ni kama shillingi Millioni 120 kufuatia bajeti zilizowasilishwa kwenye kikao hiki kutoka Idara ya Afya, Idara ya Elimu Msingi na Sekondari, Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Wadau kutoka CBDIO bado tunaendelea kujadili ili kupata bajeti halisi tutakayoenda nayo” Alisema Bi. Beatrice.
Naye, Afisa Lishe wa Mkoa wa Kagera Bi. Joanitha Jovin amesema kuwa vipaumbele vya bajeti za lishe kwa kila Wilaya vimejikita kwenye kufuata muongozo uliotolewa na Serikali Kuu ambao kwa kiasi kikubwa umetaka Elimu ya Lishe inatolewa kwa Makundi yote katika jamii. Pia kuhakikisha huduma za lishe zinapatikana na Vifaa vya kusaidia kwenye utoaji wa matibabu yatokanayo na ukosefu wa lishe bora.
Wakati akiwasilisha makadirio ya awali ya bajeti ya huduma za Lishe kwa mwaka 2025/2026 ya Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bi. Asnath Thobiath amesema kuwa bajeti hiyo imeweka baje mikakati mbali mbali ya kuhakikisha huduma za Lishe zinatolewa ipasavyo ikiwemo utoaji wa elimu kupitia majukwaa mbalimbali kama vile madhimisho ya wiki za lishe, siku ya kitaifa ya lishe, Wiki ya unyonyeshaji na Siku za kliniki za mama wajawazito. Pia kuwezesha ununuzi wa dawa za utapiamlo, kuwezesha shule kupata virutishi pamoja na kufanya madarasa ya ukarabati lishe.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.