KARAGWE DC YAADHIMISHA SIKU YA LISHE KITAIFA
Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe leo tarehe 30 Oktoba 2024 imeadhimisha siku ya Lishe Kitaifa katika viwanja vya Zahanati ya Kijiji Kiruruma kata ya Kiruruma. Maadhimisho haya yanaadhimishiwa kila mwaka tarehe 30 ya mwezi Oktoba, yakisindikizwa na kauli mbiu mbalimbali zenye kubeba ujumbe wa Lishe na ulaji wa mlo kamili ili kuepukana na udumavu katika jamii.
Kwa mwaka huu 2024, Maadhimisho ya siku ya Lishe kitaifa yamebeba kauli mbiu isemayo “Mchongo ni Afya yako, zingatia unachokula” ikiwa na lengo la kutoa elimu ya lishe kwa jamii kwa kuzingatia mapendekezo ya mwongozo wa kitaifa wa chakula na ulaji ili kuondoa dhana potofu na mitazamo hasi iliyopo kuhusu ulaji na ulishwaji wa watoto katika jamii. Maadhimisho hayo, yamembata na Utoaji wa huduma mbalimbali za Afya kama vile upimaji wa wingi wa damu kwa watoto, Presha kwa Wajawazito, ulinganisho wa Urefu na Uzito pamoja na utoaji wa elimu ya mlo kamili .
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Makamo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe na Diwani wa kata ya Chanika, Mhe: Longino Wilbard ametaka wananchi kuhakikisha wanazingatia wanacho kula na wajihusishe na shughuli za kilimo ambazo zitawawezesha kupata aina mbalimbali za vyakula ikiwemo matunda na mbogamboga, pamoja na kuzingatia maelekezo yote wanapewa na wataalamu wa Afya na Lishe .
“Niwaombe kina mama muhakikishe kwenye mashamba yenu mmepanda vyakula na matunda ambavyo ni rahisi kupatikana kwenye mazingira yetu kwa kufanya hvyo mtaweza kupata mlo kamili kwa urahisi, vibaki vile ambavyo ni vikubwa ambavyo vitalazimu kununua kama vile nyama, samaki na vingine ambavyo ni vigumu kupata kwenye mazingira yetu”. Alisema Mhe: Longino.
Naye, Ndugu Claudia Nkuba ambaye ni Kaimu Mratibu wa Lishe wa Wilaya wakati akiwasilisha risala iliyoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho hayo, ameishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa Lishe kwa wananchi na kuiadhimisha Siku ya Lishe kitaifa ili kuhimiza ulaji na kuzingatia mtindo bora wa maisha hususani ulaji wa vyakula mchanganyiko, kuepukana na matumizi ya pombe, tumbaku na bidhaa zake, pia ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni.
Kwa upande wake, Paskazia John mkazi Kiruruma ameshukuru kwa elimu aliyoipata na ameahidi kuwa balozi mzuri wa Lishe kijijini hapo na ameomba elimu hiyo itolewe mara kwa mara ili wananchi wasichukulie poa swala la lishe ambalo linaathari nyingi kiuchumi na kijamii.
Aidha, Mheshimiwa Longino ametumia maadhimisho hayo kuwasisitiza wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 pamoja na kuwakumbusha wazazi wajibu wao wa kuwapeleka watoto shuleni na kuwalea hayo kwenye misingi bora na maadili.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.