KAMBI YA SIKU 5 YA MADKTARI BINGWA WA MAMA SAMIA YAHUDUMIA WAGONJWA 508 KARAGWE DC
Kambi ya Siku 5 Madaktari Bingwa wa Mama Samia katika Hospitali ya Wilaya ya Karagwe (Nyakanongo) imehudumia wagonjwa 508.Kambi hiyo ilianza Novemba 4 hadi 9, 2024 ikiwa na madktari bingwa 7 kutoka Hospitali za Rufaa Mikoa mbalimbali Nchini kama vile Hospitali ya Bugando, Temeke , Songea, Muhimbili nakadhalika.Huduma zilitolewa ni Magonjwa ya Wanawake, Upasuaji, Meno, Magonjwa ya watoto, na Magonjwa ya ndani kama vile kisukari.
Hayo yameelezwa na Kiongozi wa msafara wa Madaktari Bingwa Dr. Edgar Ndaboine ambaye ni Daktari wa Magonjwa ya Wanawake wakati wakiagana na Madaktari wa Wilaya ya Karagwe Dr.Ndaboine ameupongeza Uongozi wa Wilaya ya Karagwe kwa kufikisha ujumbe wa ujio wa madaktari hao kwasababu muitikio umekua mkubwa na utayari wa wagonjwa katika pokea matibabu na ushauri waliopewa na wataalamu hao.
“Kwa siku tano zilizohudumu hapa Hospitali ya Wilaya tumehudumia wagonjwa 508 na kufanya upasuaji kwa watu zaidi ya 18 pamoja na kutoa Rufaa kwa wagonjwa wa kansa kwenda hospitali ya Bugando kwa matibabu zaidi. Tunaamini ujio wetu umewasaidia wananchi kupunguza gharama za matibabu pamoja na umbali wa kufuata huduma za kibingwa” alisema Dr.Ndaboine
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Bi. Happiness Msanga amewashukuru Madaktari hao kwa kuhudumia wananchi wa Karagwe na kuwaomba kuitikia wito endapo watahitajika tena kwa mara nyingine baada ya menejimenti kujadili ni namna gani wataweza kuwaalika tena lengo likiwa ni kuwahudumia wananchi pamoja na kuwapunguzia gharama. Pia amewapongeza kwa kuwaongezea ujuzi watumishi wa Hospitali ya Wilaya kupitia mafunzo waliokuwa wakiwapatia na anaamini watayatumia vizuri mafunzo hayo.
Kwa upande wake, Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Dr. Karim Abdallah amewashukuru Madaktari bingwa kwa kuwaongezea ujuzi kupitia mafunzo waliokuwa wakiwapa kila asubuhi pamoja na wakati wa utoaji huduma. Pia ameongeza kuwa, ujio wa Madktari hao umeendelea kuitangaza Hospitali ya Nyakanongo kwa Wananchi ambao pengine hawakujua kama huduma hizo zinatolewa hapo kwani Hospitali hiyo bado ni mpya ina miaka minne tu tangu ianzishwe.
Kambi ya Madaktari Bingwa wa Mama Samia kwa Wilaya ya Karagwe imehudumia Wagonjwa 508 kwa mchanganuo ufuatao, Magonjwa ya ndani 250, Magonjwa ya Wanawake 123, Magonjwa yanayohusisha upasuaji 48, Magonjwa ya watoto 44 na Meno 43.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.