Na Innocent E. Mwalo.
Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe imeunda Jukwaa la Mkakati Wa Usimamizi Wa Mazao Baada ya Kuvuna ikiwa ni kuitikia wito wa Wizara ya Kilimo kupitia mwongozo uliotolewa mwaka 2019 juu ya umuhimu wa majukwaa haya yatakayowezesha kupunguza upungufu wa mazao baada ya shughuli za uvunaji.
Semina ya uundwaji wa jukwaaa hilo ilifanyika hivi karibuni wilayani Karagwe ambapo wawezeshaji kutoka wizara ya Kilimo wakiongozwa na Bi. Daphosa Jerome ambaye ni Afisa Kilimo Msaidizi Mkuu kutoka Wizara ya Kilimo.
‘’Dhima ya jukwaa hili ni kuboresha usimamizi wa mazao baada ya kuvuna kwa kuhakisha uwepo wa mbinu na teknolojia za kupunguza upotevu nakuongeza thamani ya mazao baada ya kuvuna, kutoa motisha kwa uwekezaji katika mifumo ya masoko, pamoja na kuboresha uwezo nauratibu wa mkakati’’, alisisitiza Bi Daphosa.
Bi. Daphosa alielezea umuhimu wa jukwaa hilo kutokana na takwimu kuonesha kuwa pamoja na ukweli kamba Tanzania ina uwezo wa kuzalisha chakula kukidhi mahitaji ya taifa kwa asilimia 100, inakadiriwa kuwa asilimia 30 mpaka 40 ya kiasi hicho cha nafaka kunachovunwa hupotea bila kutumiwa na walaji kwa hiyo malengo ya jukwaa hilo ni pamoja na kujenga uelewa kwa wadau kuhusu usimamizi wa mazao baada ya kuvuna, kuimarisha uwezo wa taasisi za usimamizi wa mazao baada ya kuvuna pamoja kukusanya takwimu na taarifa za upotevu wa mazao baada ya kuvuna.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika shughuli hizo, ndugu Jackson Mwakisu aliishukuru Wizara ya Kilimo kupitia Idara yake ya Usalama wa Chakula kwa kuwa na mkakati huu wa uuundaji wa majukwaa haya ya kuahasisha kuepuka upotevu wa mazao baada ya kuvuna huku akiuelezea mkakati huo kama njia ya kuimarisha kipato cha mkulima baada ya kuvuna kutokana na hatua zitakazochukuliwa na wakulima ili kuepusha upotevu wa mazao baada ya kuvunwa.
Kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na Wizara ya Kilimo, Afisa kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, ndugu Isaya Tendega alisimamia zoezi la uundaji wa jukwaa hilo ambapo wajumbe wa mkutano huo walimchagua Sostenes Ponsian kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa hilo huku Atosha Magande akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti na Avit Theofil akichaguliwa kuwa Katibu.
Mwingine akiyechaguliwa alikuwa ni Clara Timothy ambaye alichaguliwa kuwa katibu msaidizi na hivyo basi viongozi hawa wataungana na timu tendaji itayoundwa na wataalam kutoka katika Halmashauri ya Wilaya na kwa mujibu wa mwongozo wa uundaji wa baraza hili pia wajumbe walichagua wawakilishi kutoka makundi ya wakulima ambao waliochaguliwa walikuwa ni pamoja na Anatory Chikalughai, Obed Vincent na Ernestuina Shaban na kwa upande wa asasi zisizokuwa za kiserikali wajumbe waliwachagua Innocent Kokutona na Baltazar Lutataza kuwa wajumbe wa jukwaa hilo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.