Baada ya kukiendesha kwa takribani miaka 35 Chuo cha Ufundi Studi cha Wilaya ya Karagwe (KDVTC), tangu kuanzishwa kwake mwaka 1986, hatimaye Halmashauri ya Wilaya Karagwe imekikabidhi rasmi chuo hicho kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).
Makabidhiano hayo yaliyofanywa katika eneo la viwanja vya chuo cha KDVTC, kati ya Mh. Godwin Kitonka, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya na Dkt. Pancras Bujulu, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Tanzania (VETA), ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Eilimu, Sayansi na Teknolojia, Mh. Profesa Joyce Ndalichako (Mb).
Baada ya makabidhiano hayo sasa ni dhahiri kwamba shughuli za uendeshaji na usimamizi wa KDVTC zitakuwa chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia badala ya ile ya awali ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Awali katika taarifa yake kwa Mh. Waziri wa Elimu, Sayansi naTeknolojia, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Mh. Kitonka alibainisha mafanikio kadhaa wa kadhaa yaliyofikiwa na chuo hicho tangu kuanzishwa kwake yakiwemo yale ya kuratibu, kusimamia, kuwezesha, kukuza na kutoa elimu ya ufundi na mafunzo mbalimbali mfano useremala, udereva na kompyuta.
Licha ya KDVTC kukabidhiwa kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Tanzania, kwa upande wake Bwana Peter Maduki ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Studi, alikiri kuutambua mchango mkubwa uliotolewa na Halmashauri hii kwa nyakati zote toka kuanzishwa kwa chuo hiki na kutoa maombi kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hii kuendelea kutoa msaada na ushirikiano kwa chuo hicho kila utakapohitajika mara baada ya makabidhinao hayo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mh. Brigedia Jenerali Marco Gaguti, licha ya kupongeza hatua hiyo ya makabidhiano ambayo kwa mujibu wa hotuba yake ni kwamba yalifuata taratibu zote za kisheria ikiwemo vikao mbalimbali vilivyohusisha uongozi wa wilaya ya Karagwe na mkoa wa Kagera kwa ujumla, alitoa baadhi ya changamoto kwa taasisi za VETA zilizomo katika Mkoa wa Kagera.
“Kwa kuwa mkoa wetu (Kagera), ni moja ya mikoa saba itakayopitiwa na mradi wa Bomba la kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima Uganda mpaka jijini Tanga hapa Tanzania, naushauri uongozi wa VETA kubuni kozi mbalimbali za muda mfupi ili kuwapatia ujuzi vijana wetu na hivyo kuwawezesha kupata ajira mara mradi huo utakapoanza kutekelezwa”.
Licha ya kwamba taasisi ya VETA inasimamia vyuo vitatu tu mkoani Kagera ambavyo ni Chuo cha VETA cha mkoa wa Kagera, Chuo cha VETA kilichopo katika Manispaa ya Bukoba na hiki kilichokabidhiwa hapa wilayani Karagwe, Mh. Gaguti alitoa ombi maalum kwa VETA kusimamia kwa karibu takribani vyuo vyote 15 vya ufundi vilivyopo wilayani hapa kwa lengo la kuboresha elimu.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.