DC LAIZER AONGOZA MAMIA YA WANANCHI WA KARAGWE KUAAGA MIILI YA WATU 5 KATI YA 7 WALIOFARIKI KWA AJALI YA GARI
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. Julius Kalanga Laizer leo Novemba 4,2024 ameongoza mamia ya waombolezaji kuaga miili ya watu 5 iliyotambuliwa kati ya 7 waliofariki kwa ajali ya gari iliyotokea jana tarehe 03/12/2024 katika barabara ya Kihanga-Kyaka Wilaya ya Karagwe.
Tukio la kuaga miili hiyo, limefanyika kwenye Kituo cha Afya cha Kayanga ambapo miili ya watu 5 kati ya 7 ambao ni Rumanyika Charles (25), Thereza Sebastiane (65), Amanda Alfred (3), Milembe Zion (miezi 8) na Martha Msambi (23).
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mhe.Laizer ametoa salamu za pole kwa familia zilizoondokewa na wapendwa wao pamoja na Wananchi wote wa Wilaya ya Karagwe kwa kupoteza nguvu kazi ya Taifa. Pia ametumia nafasi hiyo, kutoa rai kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri kufuata sheria za barabarani ili kuepuka ajali ambazo zinaepukika.
“Ninaelekeza vyombo vya usalama barabarani kuhakikisha watumiaji wa barabara wanafuata sheria, hatutavumilia kupoteza watu tena kwasababu ya uzembe wa madereva ifahamike kuwa, yoyote atakaeingia Karagwe ni lazima afuate taratibu wa matumizi ya barabara. Serikali imefanya juhudi za kuweka alama za barabarani ikiwemo spidi ya kuendesha pamoja na taa ili kupunguza ajali,naomba tuzingatie sheria” alisema Mhe. Laizer.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Karagwe Bi.Happiness Msanga ameungana na Wananchi wa Karagwe kufanikisha zoezi la kuaga miili hiyo pamoja na kutoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao pamoja pia ametoa wito kwa wananchi ambao hawajui ndugu yao alipo kujitokeza kutambua mwili wa mtu mmoja (Mwanamke) ambaye bado hajatambulika.
Aidha,Serekali imetoa majeneza kwa ajili ya kuhifadhi miili hiyo na mkono wa pole kiasi cha shilingi 450,000 kwa kila familia iliyopoteza mpendwa wao.
Hatahivyo, Ajali hiyo ilijeruhi watu 9 ambapo watu 8 walipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Kagera kwa matibabu zaidi na hali zao kwa sasa zimeimarika na Mmoja alipelekwa hospitali ya Wilaya ya Karagwe amesharuhusiwa. Vilevile, Uongozi unaendelea kuchukua taarifa za Majeruhi ili waweze kuwataarifu ndugu zao walipo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.