DC LAIZER AONGOZA BARAZA LA BIASHARA KARAGWE.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. Julius Kalanga Laizer ameongoza kikao cha Baraza la Wafanyabiashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe leo tarehe 7 Novemba, 2024. Baraza hilo limefanyika katika ukumbi wa Angaza Wilayani humo na kuudhuriwa na Mashirika mbalimbali ya Umma, Taasisi za Kifedha , pamoja na Wafanyabiashara wa Wilaya ya Karagwe
Baraza hilo limelenga kusikiliza kero za Wafanyabishara na kuzipatia ufumbuzi, Kupokea mapendekezo ya nini kifanyike ili kuboresha utoaji huduma na uwekezaji katika Wilaya, pamoja na kutoa maelekezo mbalimbali ya Serikali na taratibu za Halmashauri ili kuendeleza na kudumisha mahusiano mazuri baina ya Serikali na Wafanyabiashara.
Akijibu hoja mbalimbali ziliziwasilishwa na Wafanyabiashara, ikiwemo ulipaji wa Kodi ya zuio ambapo Wafanyabiashara wamekuwa wakitakiwa kulipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) badala ya wamiliki wa halali wa eneo la biashara, Mhe. Laizer amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanamikataba ya pango na kuiwasilisha mikataba hiyo kwa TRA ili kodi hizo zilipwe na wamiliki wa maeneo hayo na si mfanyabiashara.Pia ametumia baraza hilo kuwataka TRA pamoja na Halmashauri kutathimini majengo yote ya biashara ili kuweza kuwatambua wamiliki wa maeneo hayo.
Aidha, Mhe.Laizer ametoa wito kwa Wafanyabiashara kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao ya kazi ikiwemo kuhakikisha wanafunga kamera za ulinzi na kuhifadhi fedha zao kwenye Taasisi za Kifedha kama vile benki badala ya kuweka pesa nyumbani, kwasababu wanahatarisha usalama wao na mali zao.
Naye, Katibu Tawala ndugu Rasul Shandala ametumia baraza hilo kuwakumbusha wafanyabiashara wanaotumia barabara kusafirisha na kupokea mizigo kutoka sehemu mbalimbali, kuzingatia matumizi sahihi ya barabara ikiwemo viwango vya uzito wa magari vilivyowekwa ili kuepuka kuharibu miudombinu ya barabara hizo, pamoja na faini ambazo zinaweza kuwa kero kwa wamiliki wa magari ambao wakati mwingine wanakua hawajui barabara zipi wanapaswa kutumia wanapoingia Wilaya ya Karagwe.
Vilevile, Baraza hilo pia lilitoa nafasi kwa mashirika ya umma pamoja na wadau wa biashara kujibu hoja zilizowahusu ili baraza hilo liwe na tija. Baadhi ya mashirika na wadau waliopata nafasi ya kuzungumza na wafanyabiashara ni Shirika la umeme la Taifa (TANESCO), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki ya NMB na TCB.
Hatahivyo, Ndg. Shandala amepongeza Wafanyabiashara kwa kuudhuria baraza hilo na kuwashuru kwa michango yao na ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za kijamii. Na ametumia nafasi hiyo kutangaza matokeo ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 kwa Wilaya ya Karagwe ambapo Wilaya imekua ya 6 kimkoa na ya 32 Kitaifa.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.