DC LAIZER AMALIZA MGOGORO WA ARDHI ULIODUMU KWA MIAKA 10
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe: Julius Kalanga Laizer mapema leo Julai 23, 2025 amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa maeneo ya Kijiji cha Igurwa na Kata ya Igurwa na kutatua mgogoro wa Ardhi uliodumu eneo hilo kwa takribani miaka 10 sasa suluhu yake imepatikana.
Mgogoro huo umemalizika kwa maridhiano ya pande zote mbili kati ya serikali ya kijiji na Bwana Salvatory kalabamu ambapo Mkuu wa Wilaya ametoa maelekezo kwa Wataalamu wa ardhi kupima na kuweka mipaka katika maeneo waliokubaliana kumpatia bwana kalabamu na Serikali ya Kijiji.
Aidha Mh. Laizer amewahakikishia wananchi hao kutokuwa na wasiwasi na kwamba serikali ya Wilaya ya Karagwe imeamua kutumia falsafa ya "Maridhiano" (Reconciliations), ili kumaliza mgogoro huo baina ya pande mbili na kurejesha hali ya amani katika eneo hilo.
Akisoma maridhiano hayo Afisa Ardhi Wilaya ya Karagwe Ndg: Alex Japhet Mpunji amesema Machi 25, 2024 kulifanyika kikao cha maridhiano kilichoongozwa na mkuu wa Wilaya na April 2024, walitembelea eneo la mgogoro na kubaini Bwana Kalabamu Salvatory anamiliki eneo lenye ekari 351.61 badala ya ekari 80 ambayo alinunua kutoka kwa wananchi wa serikali ya kijiji hicho.
Pia timu ya wataalam ilibaini anamiliki ardhi ya sehemu ya uchimbaji wa madini yenye ekari 9.5 na aliamuliwa kubaki na ekari 9.5 kama mkataba unavyoonyesha badala 16.5 kama alivokuwa ameonyesha kwenye madai yake ambapo pia kikao cha maridhiano kiliamua kumpatia ekari 50 kutoka kwenye serikali ya kijiji badala ya ekari 80 kama alivokuwa anadai.
Kwa upande wake Salvatory kalabamu ambaye aliwahi kuwa diwani wa Kata ya Igurwa amemshukuru mkuu wa Wilaya kwa kukubali kusuruhisha mgogoro huo wa muda mrefu, ambapo aliamua kusitisha kesi mahakamani ili kupata suruhisho kutoka kwake na serikali ya Kijiji.
Naye Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Karagwe Ndg: Victor Lesuya, amesema Dira ya TAKUKURU ni kutokomeza vitendo vya rushwa na kusema katika mgogoro huo, isingekuwa busara ya Mkuu wa Wilaya ya kutumia maridhiano basi watu wote wangekuwa katika mikono ya takukuru kwa uchunguzi na hatua zaidi zingechukuliwa kwakuwa Mgogoro ulikuwa unaeleza ekari 80 baada ya kupimwa zikakutwa 361 na Takukuru ikibaini hivyo inakuwa na makosa ya matumizi mabaya ya madaraka, nyaraka za kugushi na kuwasilisha nyaraka za uwongo ili kummilikisha mtu mwingine pamoja na kosa la ukwepaji kodi (utakatishaji).
Ameongeza kuwa Ardhi haiuzwi kiholela hivyo kila mmoja anapaswa kufuata utaratibu ili kupatikana kwa kodi ya serikali.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.