BOT YATOA MAFUNZO YA FEDHA NA UWEKEZAJI KARAGWE DC.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa mafunzo ya fedha na Uwekezaji kwa Wastaafu, Watumishi, Viongozi wa Vyama vya Ushirika na Watoa huduma za fedha wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
Mafunzo hayo yamelenga kueneza Majukumu ya Benki kuu ya Tanzania (BOT) ikiwemo kuhakikisha utulivu wa maswala ya uchumi, Kutambua alama za usalama wa noti na sarafu, Utunzaji wa fedha na utoaji huduma za fedha pamoja na namna sahihi ya kufanya uwekezaji, mafunzo hayo yamefanyika leo Februari 10, 2025 kwenye Ukumbi wa Halmashauri (ANGAZA).
Akiongoza Mafunzo hayo, Meneja Fedha na Utawala (BOT) Tawi la Mwanza Ndg. Meso Gaitoti amesema kuwa Benki kuu ya Tanzania inatambua kuwa swala la fedha ni nyeti hivyo ni vyema elimu ikatolewa kwa makundi mbalimbali ya watu nchini ili kuwajengea uelewa katika masuala ya kutambua alama za usalama wa fedha, Utunzaji na fursa za uwekezaji pamoja na sababu za ubadilishwaji wa fedha kwenye mzunguko.
Aidha, Ndg. Gaitoti alitumia nafasi hiyo kusisitiza Wananchi kubadilisha fedha ambazo hazitatumika tena kwenye malipo au kubadilishwa na benki Nchini kuanzia Aprili 6, 2025 kwa sababu hazitakua halali na zitaondolewa kwenye mzunguko ambazo ni shilingi 20, 200, 500, 1,000, 2,000, 5,000 na 10,000 kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi 2003, pamoja na noti ya shilingi 500 ya mwaka 2010.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Ndg. Wilson Nyamunda amewashukuru wawezeshaji kutoka BOT kwa mafunzo na kuwataka waliopata mafunzo hayo kuyafanyia kazi ikiwemo uwekezaji pamoja na kuwafikishia ujumbe wengine ili mafunzo hayo yawe na tija kwenye jamii nzima ya Karagwe.
Vilevile, Washiriki wa mafunzo walipata wasaa wa kuuliza maswali mbalimbali kufuatia mada zilizowasilishwa na wakufunzi kutoka BOT ambapo moja ya swali lililoulizwa ni kuhusu mikopo ya kaushadamu na kuomba mafunzo kama haya kutolewa mara kwa mara kwani yanaleta tija kwa jamii.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.