Na Innocent E. Mwalo.
Mashindano ya mpira wa miguu maarufu kama ‘’Ligi ya Bashungwa’’ ambayo hufanyika kila mwaka wilayani hapa kwa udhamini wa mbunge wa jimbo la Karagwe ambaye pia ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mh. Innocent Lugha Bashungwa, Julai 4, 2021, yameanza kurindima katika uwanja wa Bashungwa uliopo mjini Kayanga.
Mechi ya ufunguzi iliyochezwa katika siku ya kwanza ya mashindano haya ilikuwa ni baina ya timu za kata ya Nyakahanga na Kamagambo, ambapo timu ya Kamagambo iliibuka mshindi kwa goli moja, dhidi ya timu ya Nyakahanga, bao lililofungwa dakika ya 28 ya kipindi cha kwanza cha mchezo na mchezaji wa timu hiyo ya Kamagambo ajulikanae kwa majina ya Jovinus Ludovick.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa mashindano haya alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mh. Juliet Binyura ambaye aliambatana na kamati ya ulinzi ya wilaya huku wageni wengine wakiwa ni mwenyekiti wa Halmsaharui ya Wilaya Mh. Wallace Mshanda pamoja na baadhi ya madiwani kutoka katika kata mbalimbali za wilaya Karagwe.
Mh. Binyura licha ya kupongeza mafanikio ambayo timu ya Kamagambo waliyapata katika mchezo huu wa siku, pia alitumia wasaa huo kuzitaka timu zote zitakazoshiriki katika mashindano hayo kudumisha nidhamu na upendo wakati wote wa mashindano hayo.
‘’Naomba kusisitiza kwamba licha ya ushindani mnaotakiwa kuuonesha lakini ni lazima mjue dhumuni jingine la michezo ni kuwakutanisha kwa ajili ya kujenga urafiki na udugu miongoni mwao’’, alisema Binyura.
Mashindano haya yanayozishirikisha timu kutoka katika kata zote 23 za wilaya ya Karagwe, yanatarajiwa kudumu kwa takribani miezi miwili ambapo mshindi katika katika mashindano haya anatarajiwa kukabidhiwa zawadi na tuzo na Mh. Bashungwa mapema mwezi Septemba mwaka huu.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.