BARAZA LA WAHESHIMIWA MADIWANI KARAGWE DC LARIDHIA BAJETI YA SHILINGI BILLIONI 53.8 KUTUMIKA KWA MWAKA WA FEDHA 2025/2026.
Baraza la Waheshimiwa Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe limepitisha mpango wa bajeti wa shilingi Billioni 53.8 kutumika kwenye Halmashauri kwa mwaka fedha 2025/2026. Bajeti hii imepitishwa baada ya kujadili mapendekezo na vipaumbele vilivyowasilishwa kulingana na makadirio ya mapato ya ndani pamoja na vyanzo vingine ikiwemo ruzuku kutoka Serikali kuu.
Akifungua baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mhe.Wallace Mashanda amesema kuwa sehemu ya bajeti iliyopitishwa kwa mwaka 2025/2026 imelenga kuongeza vyanzo vya mapato kwa Halmashauri ili mapato hayo yatumike kufanikisha miradi mbalimbali yenye tija kwenye jamii.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe.Julius Kalanga Laizer amewataka wajumbe wa baraza hilo kusimamia miradi iliyowasilishwa kwenye bajeti ili iweze kutoa huduma kwa Wananchi wa Karagwe pamoja na kuiongezea Halmashauri mapato. Pia amesisitiza bajeti hiyo iliyopitishwa itoe kipaumbele kwa miradi viporo kwa kijamii kama vile maabara za shule na vituo vya Afya ili huduma zianze kutolewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Bi.Happiness Msanga amesema kuwa bajeti iliyowasilishwa imefuata muongozo wa vipaumbele ulitolewa na Serikali kwa mwaka 2025/2026 ikiwemo kuzitaka Halmashauri zote kutenga bajeti kwa kuzigatia ujenzi wa miundombinu wezeshi na kuimarisha matumizi ya Tehama, kupima maeneo ya Serikali na Taasisi za umma, Kumalizia miradi viporo na iliyoanzishwa na Wananchi, Kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi maalum, kulipa fidia pamoja na kuanzisha miradi ya kimkakati ya kuiongezea Halmashauri mapato na kunufaisha Wananchi.
Akiwasilisha mchanganuo wa bajeti ya kiasi cha shillingi billioni 53.8 kwa niaba ya Mkurugenzi, Afisa Mipango Bw. Cyliacus Felician amesema kuwa fedha hizo zitatumika kuendeleza miradi ya kuongezea mapato Halmashauri ikiwemo ujenzi wa shule ya mtaala wa kingereza, ujezi wa kituo cha afya, kufanya tamthimini ya miradi mikakati, Kupima na kurathimisha ardhi kwenye mji pamoja na ujenzi wa shule ya sekondari bashungwa na maabara katika baadhi ya shule za sekondari wilayani humo.
Hatahivyo, kupitia baraza hilo la Madiwani la kujadili na kupitisha bajeti Mkurugenzi Mtendaji Bi.Happiness alitoa taadhari ya Ugonjwa wa Marburg ambao umethibitishwa kuwepo mkoa wa kagera (Biharamulo) ambapo aliwasihi wajumbe kuendelea kuchukua taadhari na kuwapa elimu wananchi ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa huo japokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe haina mgonjwa mwenye maambukizi ya ugonjwa huo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.