BARAZA LA MADIWANI WAJA NA MPANGO MKAKATI WAKUHAMASISHA WANANCHI KULIMA MAZAO YA UKAME
Mkutano wa Baraza la Madiwani robo ya kwanza la mwaka 2024/2025 (Mwezi Julai hadi Septemba) katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe uliofanyika Novemba 12 na 13, 2024 limeweka mpango mkakati wa kuhamasisha Wananchi kulima mazao yanayostahimili ukame ili kupambana njaa itakayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo ukosefu wa mvua za kutosha kipindi cha Vuli.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe na Diwani wa Kata ya Nyaishozi Mhe. Wallace Mashanda amezungumzia uhaba wa mvua Wilaya ya Karagwe kwa mwaka huu, ambapo kupitia mkutano huo wa siku mbili Baraza la Madiwani limeazimia kushirikisha viongozi wote ndani ya Wilaya wakiwemo Viongozi wa dini, Mashirika na Watendaji wa Serikali kuweka mikakati ya kuweka mkazo kwa wananchi kulima mazao yanayostahimili ukame kama vile mihogo na viazi, Pamoja na kuwakumbusha wazazi wenye watoto wanaosoma kuandaa mazao ya chakula mapema kwaajili ya wanafunzi ili mwaka wa masomo utakapoanza watoto waweze kupata chakula shuleni.
Akitoa maelekezo ya Serikali katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. julius Kalanga Laizer amewaomba Waheshimiwa Madiwani, Wadau wa Serikali na Wananchi kuhakikisha Ulinzi na Usalama wa Wilaya unazingatiwa kwa asilimia mia hasa kipindi cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2024. Pia alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa Wananchi kuacha kukata miti kwa ajili ya mkaa ikibidi Wilaya itafute namna ya kupunguza vibali vya kukata miti ili kuepukana na ukame.Alizungumzia pia kuhusiana na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa wananchi ambapo aliutaka Uogozi wa Halmashauri kutoa mafunzo kwa viongozi hususani madiwani ili waweze kufikisha ujumbe sahihi wa mikopo hiyo na kumbushia wadeni kulipa madeni yao ili wengine waweze kukopa.
Naye, Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo La Karagwe Mhe.Innocent Bashungwa wakati akitoa salamu kwenye mkutano huo, Amesema kuwa Serikali inatarajia kuleta kivuko kwenye Ziwa Burigi ili kurahisisha usafiri kwa wakazi wa kijiji cha Ruhita, Mililo na Kigasha ambapo kwa miaka mingi wamekua wakipata changamoto ya usafiri ambapo iliwalazimu kutumia boti ambazo zinahatarisha usalama wao na mali zao. Pia amewapongeza Madiwani kwa kazi nzuri wanazofanya kwenye kata zao na kutumia nafasi zao kuwaelimisha Wananchi waachane na imani potofu.
Aidha, Waheshimiwa Madiwani wa Kata zote 23 za Wilaya ya Karagwe walipata nafasi ya kuwasilisha taarifa za Kata zao kuanzia Julai hadi Septemba kwa mwaka 2024, Pamoja na kuwasilisha taarifa za Kamati za kudumu za Halmashauri. Wakizungumza kwa nyakati tofauti za uwasilishaji wa taarifa hizo Madiwani walisema kuna uhaba wa mvua jambo ambalo liliwekewa azimio la kupanda mazao yanayostahimili Changamoto nyingine zilizowasilishwa na Waheshimiwa Madiwani ni kuhusu makusanyo ya Mapato kwenye vizuizi na uchache wa watumishi baadhi ya maeneo.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Ya Karagwe Bi.Happiness Msanga wakati akijibu maswali ya papo kwa papo na hoja zilizowasilishwa kwenye taarifa za Kata za Madiwani amesema kuwa Makusanyo ya vizuizi vya Wilaya ya Karagwe wakusanywe kulingana na eneo la utawala na alisisitiza makusanyo yoyote ya kwenye Kata yanatakiwa kupelekwa benki kabla ya kupangiwa matumizi. Kuhusu Uhaba wa Watumishi, Mkurugenzi amesema kuwa, Halmashauri itazingatia msawazo wa watumishi waliopo na kuendelea kuomba Watumishi Serikalini Pia alitoa wito kwa Waheshimiwa Madiwani kuwahamasisha Wananchi kujenga nyumba bora ya kupangisha ili Watumishi wanapopangiwa maeneo hayo waweze kupata makazi.
Aidha, Mkutano huo ulitoa nafasi kwa Mashirika ya Umma kuwasilisha taarifa za utelekelezaji wa miradi yao kulingana na bajeti na kutoa majibu ya hoja ambazo zimeibuliwa na Waheshimiwa Madiwani wakati wa uwasilishwaji wa taarifa za kila Kata. Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) ni moja ya Shirika la Umma lililowasilisha taarifa yake na kujibu hoja zilizoibuliwa kuhusiana na barabara mbalimbali Wilayani humo ikiwemo Bukangaro. Mkurugenzi wa TARURA wilaya ya Karagwe aliwaomba Waheshimiwa Madiwani kuwasilisha changamoto na barabara zitakazopewa kipaumbele kabla ya bajeti ya mwaka mpya itakayopangwa Disemba 2024.
Hata hivyo, Mkutano huo ulipata ugeni kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambao walifanya mafunzo mafupi kwa ajili ya kukumbushia Sheria na Maadili kwa Viongozi na Watumishi wa Umma.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.