Wilaya ya Karagwe Yaitikia Agizo la Makamu wa Rais Juu Ya Utunzaji wa Mazingira.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Katika kuitikia kwa vitendo agizo lililotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan Desemba 22, 2017 mjini Dodoma wakati alipozindua Kampeni kabambe ya kuufanya mkoa huo kuwa wa kijani, Wilaya ya Karagwe imetekeleza kwa vitendo agizo hilo kwa kushiriki kikamilifu katika upandaji wa miti takribani 350 katika viunga vya mji wa Kayanga.
Tukio hilo la kihistoria lilifanyika mnamo tarehe 30 Desemba, 2017 ambapo kikundi kiitwacho Karagwe Great Mind alimaarufu kama (Timu Ten Ten) wakishirikiana na Idara ya Mazingira na Taka Ngumu ya Halmashauri ya Wilaya Karagwe kwa pamoja waliweza kuandaa hafla hiyo ya upandaji wa miti takribani 350 zoezi lililoenda sambamba na kufanya usafi katika Kituo cha Afya cha Kayanga.
Mgeni rasmi katika Hafla hiyo alitarajiwa kuwa Mh. Godfrey Mheluka ambaye hata hivyo kutokana na kuwa nje ya wilaya kwa shughuli za kikazi hakuweza kushiriki zoezi hilo kazi iliyofanywa kwa niaba yake na Katibu Tawala wa Wilaya Mh. Innocent Nsena ambaye alikuwa ameongozana takribani na wajumbe wote wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya.
Katika maeneo yote ambapo upandaji wa miti ulifanyika wananchi katika Taasisi na maeneo hayo walikabidhiwa kwa maandishi kutunza miti hiyo kwenye maeneo hayo.
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi katika kushiriki katika zoezi hilo, Mlezi wa kikundi hicho cha Karagwe Great Mind ndugu Karrim Amri aliwashukuru wananchi walioshiriki katika zoezi hilo ikiwa ni ishara ya kuunga mkono kampeni hiyo.
“Mh. Mgeni rasmi kikundi chetu kina wananchama 26 ambapo kinajihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo utunzaji wa mazingira na katika kuonesha hilo tumeamua kuunga mkono jitihada za Makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan alizozifanya hivi karibuni katika zoezi la upandaji wa miti”, alisema ndugu Karrim.
“Pamoja na kwamba kikundi chetu ni kichanga lakini tumeweza kutumia kiasi cha Tsh.350,000 katika zoezi hili na kwa kweli tunaomba ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya zinatupa sana ushirikiano lakini bado tunayo changamoto ya kukosa ofisi”, alisisitiza ndugu Karrim.
Kwa upande wake Mgeni rasmi, Katibu Tawala Wilaya Mh. Innocent Nsena pamoja na kusoma hotuba iliyoandaliwa na Mkuu wa Wilaya aliwashukuru wanakikundi hicho na kuwaahidi kwamba wilaya inatambua mchango mkubwa wanautoa kwa jamii na akawahakikishia kwamba daima wilaya itaendelea kuwathamini kwa mchango wa hali na mali wanaoutoa.
“Ofisi ya Mkuu wa Wilaya inatambua kwamba pamoja na kikundi chenu kuwa bado ni kichanga lakini mmekwisha shiriki kwa hali na mali kwa mambo kadhaa ya kijamii na kwa kweli mnastahili pongezi na niwahakikishie kuwa ofisi yetu ipo tayari kwa chochote mtakachohitaji kutoka katika ofisi zetu”, alisema Mh. Nsena.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.