“SERIKALI KUJENGA HOSPITALI WILAYANI KARAGWE 2018/2019”, JAFO
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE..
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mh. Suleiman Jafo (MB), mnamo Mei 11, 2018 amewatangazia wananchi Wilayani Karagwe ya kwamba Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 105 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali 67 hapa nchini ambapo Wilaya ya Karagwe ni miongoni mwa Wilaya hizo zitakazojengewa miundombinu ya hospitali hizo.
Mh. Jafo alibainisha haya kwa nyakati tofauti alipowahutubia wananchi Wilayani hapa kwenye maeneo ya Shule ya Msingi Ihembe na kwenye kituo cha Afya cha Kayanga katika ratiba yake ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani hapa na mkoani Kagera kwa ujumla.
“Naomba niwaambie wananchi wa Karagwe ya kwamba serikali inakwenda kufanya historia kwa kujenga hospitali 67 kwa muda mfupi na hayo yatakuwa maendeleo makubwa kuwahi kutokea hapa nchini kwenye sekta ya afya takwimu zinaonesha ya kwamba toka nchi yetu ipate uhuru ni hospitali takribani 77 tu zimejengwa nchini kote”, alisisitiza Mh. Jafo.
Licha ya kusisitiza masuala mengine katika sekta ya afya ikiwemo azima ya serikali kuajiri zaidi ya watumishi 6,000 wa sekta ya afya hapa nchini, Mh. Jafo alitoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya kuwakopeshwa wananchi pesa za vikundi bila kuwatoza riba.
Katika hatua nyingine Mh. Jafo alipata nafasi ya kutembelea miradi miwili ya maendeleo wilayani hapa ikiwemo kufanya uzinduzi na kuweka jiwe la msingi ambapo mradi wa kwanza aliozindua ulikuwa ni ule wa ukarabati wa vyumba vitano vya madarasa, stoo tatu na ujenzi wa matundu nane ya vyoo katika shule ya Msingi Ihembe, miradi ambayo hadi kukamilika kwa ujenzi wake itagharimu kiasi cha 66,600,000 ikiwa ni gharama zilizotolewa kwa asilimia mia moja na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikiwa ni kutekeleza ahadi ya waziri huyo aliyoitoa mnamo 25/07/2071 alipofika kwenye maeneo hayo kwa ziara ya kikazi iliyokuwa na lengo la kuzindua jengo la utawala lenye chumba kimoja cha darasa na ofisi mbili.
Katika taarifa kwa waziri huyo ilionesha ya kwamba wa miundombinu hiyo uj umefanywa kwa kutumia mwongozo wa sheria ya manunuzi maarufu kama “force account”
Mapema katika taarifa iliyosomwa na Mwalimu Mkuu kwenye Shule hiyo ya Msingi Ihembe, Mwalimu Vaston Rugaju, taatifa hiyo iliainisha ya kwamba pamoja na kukamilika kwa ujenzi huu, kuna mambo hayakukamilika kutokana na fedha hiyo kutokutosheleza ikwemo kuweka mfumo wa maji vyooni unaotarajiwa kugharimu kiasi cha 7,535,000/= ambapo hata hivyo Mh. Waziri Jafo aliagiza Halmashauri ya Wilaya kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kukamilishwa kwa ujenzi wa miundombinu hiyo.
Aidha mradi mwingine ambao Waziri Jafo aliweka jiwe la msingi ilikuwa ni ule wa ujenzi wa miundombinu katika kituo cha Afya Kayanga.
Kwenye mradi huu, serikali ilitoa jumla ya 170,714,452.18 mnamo mwaka 2017 kwa ajili ya kuiwezesha Halmashauri ya Wilaya kufanya ukarabati wa miundombinu katika kituo cha afya hicho kufuatia miundombinu yake kuathiriwa na tetemeko la ardhi lilitokea mnamo Septemba 11, 2016 na kusababisha madhara makubwa kwa miundombinu mbalimbali ikiwemo ile ya serikali ambapo kwa kutumia fedha hizo serikali iliweza kujenga wodi ya wazazi ambayo sasa inatumika kama wodi ya watoto, chumba cha kuhifadhia maiti na kiasi kingine kinachobaki kiliweza kutumika kwa ajili ya ujenzi wa power house.
Kadhalika kituo hiki cha afya kiliweza kupokea kiasi cha 72,789,530 na vifaa vya ujenzi kutoka ghala la maafa la mkoa vilivyofanya kazi kuezekea wodi ikiwa ni kutimiza ahadi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana na wenye ulemavu aliyotoa kufuatia ziara yake wilayani hapa mnamo Julai 13, 2017.
“Aidha katika hatua nyingine, Halmashauri iliweza kupokea kiasi cha 500,000,000/= kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kituo cha afya Kayanga ambazo zilitumika kujenga jengo la wagonjwa wan je, nyumba ya mganga, wodi ya wazazi, chumba cha upasuaji, jengo la utawala na ‘walk ways’”, ilibainishwa kupitia taarifa iliyosomwa kwa Waziri Jafo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.