Waziri Mwigulu apamba Masindano ya Ligi ya Bashungwa, Mamia Wafurika Uwanja wa “Push- Up”
Na Innocent E. Mwalo, Karagwe.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameyapamba mashindano ya Ligi ya Mbunge wa Karagwe Mh. Innocent Lugha Bashungwa alimaarufu kama “Bashungwa Clup Cup” yaliyomalizika jioni ya tarehe 08/10/2017.
Mashindano haya yaliyoanza mapema mwezi Agosti, yamedumu kwa takribani miezi miwili (02) na yamechukua takribani miezi mitano (05) ya maandalizi.
Kadhalika mashindano haya yalihusisha kata zote ishirini na tatu (23) za wilaya ya Karagwe huku Kata ya Ihembe ikiwa ndio bingwa wa shindano hili kufuatia mtanange wake na timu ya Nyaishozi iliyogaragazwa kwa magoli mawili na timu hiyo ya Ihembe katika mchezo huo wa fainali.
Mapema kabla ya kukipiga kwa timu hizi za Nyaishozi na Ihembe, wananchi wengi walitabiri mchezo huo kuwa mgumu kufuatia umaarufu wa kila timu, kutambiana kwa timu hizo na rekodi ya kichapo ambacho timu hizi zilikisambaza kwa timu ilizokutana nazo kwenye robo fainali na nusu fainali.
Mapema Waziri Mwigulu alipowasili Wilayani Karagwe alipokelewa na mwenyeji wake Mh. Innocent Lugha Bashungwa aliyekuwa ameambatana na viongozi kadhaa wa chama cha Mapinduzi na Jumuiya zake.
Baada ya kusalimiana na na viongozi hao, Waziri Mwigulu alisalimiana na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya Karagwe Mh. Godfrey Ayubu Mheluka, Wheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, Wataalamu toka Halmashauri ya Wilaya wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hamashauri ya Wilaya hii, ndugu Ashura Kajuna.
Kisha Mheshimiwa Waziri Mwigulu alifanya kikao kifupi na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kabla ya kuelekea uwanjani wa changarawe uliopo mjini Kayanga kwa minajili ya kushuhudia mtanange huo.
Baada ya kupokelewa na Halaiki ya skauti Mh. Nchemba alipata nafasi ya kushuhudia mtanange kati ya Timu za Kata za Kiruruma na Nyakakika zilizokukuwa zinakabana koo kwa lengo la kumtamfuta mshindi wa tatu katika mashindano hayo ambapo timu ya Kiruruma iliweza kuibuka mshindi wa pili kwa kuiburuza timu ya Nyakakika kwa mabao mawili kwa sifuri.
Baada ya mtanange huu, ndipo risala ilisomwa kwake Mh. Waziri na mratibu wa Mashindano haya ya “Bashungwa Club Cup” na kisha ikafuatiwa na salamu kutoka kwa Mh. Waziri Mwigulu ambaye pia ndiye Raisi wa Klabu ya Mpira wa miguu mkoani Singida ijulikanayo kama “Singida United”
Katika hotuba yake Mh. Waziri Mwigulu aliiahidi timu kuifadhili klabu hii ya Bashungwa kwa ajili kwenda kupambana na Klabu ya Singida United lengo likiwa ni kuitangaza Klabu hii ijulikane na hivyo basi kuwafanya wawezaji wa soka hapa nchini kuona vipaji vinavyochipuka kwa ajili ya kuvikuza.
Katika mashindano haya alikuwepo pia Kocha wa Timu ya Kagera Sugar, Mecky Maximo ambaye alikuja mahususi kwa ajili ya kuangalia vipaji vinavyochipukia na ndiye aligawa zawadi kwa washindi kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mh. Bashungwa alipopata nafasi ya kumshukuru Mh. Waziri Mwigulu, kwanza alimwagia sifa kemkem kutokana na Waziri Mwigulu kumwaliki Mh. Bashungwa kwenda jimboni kwake Iramba Magharibi kwa ajili ya kujifunza mambo kadhaa wa kadhaa ukizingatia kwamba hiki ni kipindi cha pili cha Ubunge kwa Waziri Mwigulu ukilinganisha na kipindi cha kwanza cha Mh. Bashingwa ambapo daima anakuwa anajifunza mambo mengi mengikwa waliomtangulia kutokana na ugeni wake na umri wake wa ubunge.
“Nakushuru sana kaka yangu Mwigulu kwa namna unavyoniongoza na kunisaidia katika kujifunza nakumbuka miezi kadhaa iliyopita ulinialika name nikashiriki katika ziara yako jimboni kwako Iramba Magharibi ambapo nilijifunza mambo kadhaa hasa uanzisaji wa Ligi hizi”, alisema Bashungwa akishangiliwa na umati uliofurika katika uwanja wa changarawe Mjini Kayanga alimaarufu kama “uwanja wa Pus- up”.
“Napenda kuwashukuru nyote kwa kushiriki mashindano haya na kipekee madiwani wenzangu ambao mlitengeneza hamasa na utaratibu kwenye kata zenu na kufanya kata zenu zote kushiriki kikamilifu”, alisema Bashungwa.
Mh. Bashungwa alizitaja faidha kadhaa za mashindano kama hayo kwamba licjha ya kwamba yanawaunganisha wananchi na kuwafanya kuwa pamoja; mashindano hayo yamehamasisha hulka ya watu kufanya kazi kwani yamekuwa yakifanyika muda wa mchana baada ya kazi na kuwafanya wananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali muda wa asubuhi.
Mashindano kama haya yanatajwa kuwa ni ya kudumu katika kipindi hichi cha Ubunge wa Mh. Bashungwa kwani yatakuwa yakifanyika kila mwaka ili kuweza kuwajegea vijana uwezo wa kushiriki katika kukuza vipaji kwani mashindano haya yakitangazwa vyema hii inaweza kuwa fursa ya kutangaza na kuibua vipaji vya wachezaji wa mpira wa miguu kwa vijana waliyopo katika wilaya ya Karagwe.
Katika mashindano haya timu ya Ihembe iliyoibuka mshindi ilipewa zawadi ya kombe lenye thamani ya Tsh. Milioni moja na kukabidhiwa kiasi cha fedha tasilimu cha shilingi milioni moja na nusu.
Mshindi wa pili timu ya Nyaishozi ilipewa kiasi cha shilingi laki saba na elfu Hamsini na mshini wa tatu ambaye ni kata ya Kiruruma akipewa kiasi cha shilingi laki nne huku mshindi wanne ambaye ni timu ya Nyakakika ikipewa kiasi cha shilingi laki mbili.
Kadhalika timu zote kutoka katika kata 23 za wilaya Karagwe zilipewa mpira mmoja mmpja na jezi zilizogawiwa mapema kabla ya kuanza kwa ligi hiyo mwezi Agosti.
Katika Mkutano huo mbunge huyu wa Karagwe aliibua changamoto ya bodadoda kunyanyaswa na askari wa usalama barabarani na waziri wa mambo ya ndani ya nchi alitoa maelekezo kwa wasimamizi hao wa sheria kutowanyanysa waendesha bodaboda hao kwa makosa ambayo sio yao mfano kama kosa ni la mmiliki wa chombo basi kwa maelezo ya Mhe. Waziri anayepaswa kushughukiliwa ni mmliki wa chombo na si mwendesha bodaboda kama ilivyozoeleka.
“Hali kadhalika, kwa abiria anayepanda chombo hicho naya anapaswa kushughulikiwa binafsi kwa makosa yake kama atabainika kuvunja sheria”, alisisiza Mh. Mwigulu kupitia hadhara hiyo.
Kwa namna nyingine Waziri Mwigulu aliahidi kurudi tena mkoani Kagera na Wilayani Kargwe kwa lengo la kuja kufanya ziara rasmi ya kikazi Wilayani humu ambapo atapata nafasi ya kuzungumzia zaidi pamoja na kuyatolea ufafanuzi mambo kadhaa yahusuyo wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.