WAZIRI MKUU MH. KASSIM MAJALIWA MAJALIWA AFANYA ZIARA YA KIHISTORIA WILAYANI KARAGWE NA KUTANGAZA NEEMA LUKUKI
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), mnamo Oktoba 07, 2018 amefanya ziara ya kihistoria Wilayani hapa huku akitangaza neema kadhaa kwa wananchi wa Wilaya hii.
Ikiwa ni siku ya pili katika ziara yake ya kikazi itakayodumu kwa takribani siku nne hapa mkoani Kagera, Waziri Mkuu Mh. Majaliwa amezuru wilaya ya Karagwe akitokea wilaya ya Kyerwa ambapo mara baada ya kuwasili wilayani hapa alilakiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya chini ya Mwenyekiti wake ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mh. Godfrey Mheluka.
Mara baada ya mapokezi hayo ugeni huo ulienda moja kwa moja kutembelea Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha KADERES kinachomilikiwa na ndugu Leonard Kachenabo ambapo akiwa kiwandani hapo Waziri Mkuu, Mh. Majaliwa alisifu jitihada za mwekezaji huyo katika kuitikia kwa vitendo kauli ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli juu ya utekelezwaji kwa vitendo kwa sera ya viwanda hapa nchini.
Aidha, ziara hiyo ilielekea katika Kituo cha Afya Kayanga ambapo Waziri Mkuu alifanya ukaguzi wa ujenzi wa Miundombinu ya Kituo cha Afya cha Kayanga kikiwa ndio kituo kikubwa cha Afya Wilayani hapa chenye uwezo wa kuhudumia wananchi takribani 2,400 mpaka 3,500 kwa mwezi.
Katika ukaguzi huo ulioenda sambamba na kuwajulia hali wagonjwa, Waziri Mkuu Mh. Majaliwa pamoja na ujumbe aliokuwa ameambatana nao waliridhika na ujenzi wa miundo mbinu katika kituo hicho ambapo takwimu zinaoonesha kuimarika kwa huduma zote za muhimu ikiwemo huduma ya upasuaji iliyoanza kutolewa tarehe 08/12/2016.
Itakumbukwa kwamba, Kituo hiki cha afya kilipokea kiasi cha Tsh.170,714,452.18 mnamo 16/06/2017 kutoka Mfuko wa Maafa wa Mkoa kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi, chumba cha kuhifadhia maiti na power house; fedha ambazo zilipelekwa moja kwa moja katika kituo hiki cha afya kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kwa kutumia utaratibu wa “Force Account”
Kadhalika, Halmashauri ya Wilaya Karagwe ilipokea kiasi cha Tsh. 500,000,000 kutoka Serikali kuu chini ya mradi wa kuboresha vituo vya afya ikiwa ni kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa majengo wa Kituo cha Afya cha Kayanga kwa ufadhili wa Serikali ya Canada, fedha ambayo imetumika katika ujenzi ujenzi wa wodi ya akina mama, nyumba ya mtumishi, jengo la huduma za wagonjwa za afya ya uzazi na mtoto pamoja na huduma za wagonjwa wa nje (OPD na RCH) na jengo la wodi ya wanawake ambapo miradi yote hii ilikaguliwa na Waziri Mkuu.
Ziara ya Waziri Mkuu ilihitimishwa katika Uwanja wa Changarawe alimaarufu kama Uwanja wa “Push Up” ambapo umati wa wananchi ulimlaki na kumsikiliza Waziri Mkuu, Mh. Majaliwa ambaye alitumia hadhara hiyo kueleza mipango ya serikali kwa Wilaya ya Karagwe na Mkoa wa Kagera kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kujibu maombi na michango mbalimbali ya wabunge akiwemo Mbunge wa Karagwe Mh. Innocent Lugha Bashungwa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera Mh. Oliva Semguruka ambao kwa nyakati tofauti walitumia fursa waliyoipata kusalimia wananchi katika kufikisha kilio cha wananchi wa Karagwe kuhusu kero za maji, umeme, barabara, upungufu wa watumishi hasa katika kada za afya na tatizo la ununuzi wa kahawa ambapo kila lilipogusiwa wanachi walishangiliwa wakitajia kupata majibu kutoka kwa Waziri Mkuu aliyekuwa pia ameambatana na Waziri wa Kilimo, Mh. Dkt. Charles Tizeba.
Hata hivyo kabla ya kujiwa kwa baadhi ya hoja na Waziri Mkuu, Waziri wa Kilimo, Mh. Dkt. Tizeba alitangaza azima ya serikali juu ya kuondoa agizo la kuomba vibali vya kununua kutoka Halmashauri ambapo kwa sasa wanunuzi wa kahawa watapaswa kuwa tu na leseni ya biashara; lengo likiwa kupunguza urasimu usiokuwa na tija.
Waziri Mkuu alizitolea majibu baadhi ya hoja zilizotolewa na waheshimiwa wabunge na kutoa maagizo kadhaa ya serikali ikiwemo kuwaagiza watumishi wa Halmashauri ya Wilaya kuwapokea vizuri wananchi, kuwasikiliza, kuwahudumia na lililo kubwa likiwa kwenda vijijini wanakapatikana wanachi wanyonge wasio na uwezo wa kusafiri umbali kufika wilayani kwa ajili ya kwenda kusikiliza na kutatua kero zao ambazo zipo ndani ya uwezo wao watumishi hao wa Halmashauri ya Wilaya.
“Aidha nawaagiza Halmashauri ya Wilaya kusimamia kikamilifu miradi ikiwemo kutekeleza kwa vitendo agizo la serikali la kuhakikisha kila kijiji kinajenga zahanati ambapo waheshimiwa madiwani na menejimenti ya wilaya mnao wajibu wa kuhamasisha jamii juu ya utekelezaji wa agizo”, alisema Mh. Majaliwa
“Kadhalika nakubalina na maombi ya mbunge wenu Mh. Bashungwa juu ya kujengwa kwa vituo vya afya katika maeneo ya Bushangaro na Kituntu ambapo niwahakikishe kwamba jambo hili litatekelezwa katika awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huu wa ujenzi wa vituo vya afya”, alisema Mh. Majaliwa huku akishangiliwa na wanachi waliokuwa wamekusanyika kumsikiliza.
Kuhusu miradi ya maji, Waziri Mkuu aliwatoa hofu wananchi juu ya utekelezwaji wa mradi wa BUWASA ambao utekelezwaji wake umesimama kuanzia mwezi Februari 2018 ambapo alisema tayari serikali imeshashughulikia malipo ya mkandarasi wa mradi huu na mradi huu utatekelezwa hivi karibuni.
“Lakini serikali ina mpango wa kuipatia ufumbuzi kero hii ambapo zaidi ya jumla ya shilingi bilioni 370 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Rwakajunju kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Wilaya ya Karagwe”, alinukuliwa Waziri Mkuu.
Ufafanuzi mwingine aliotoa Waziri Mkuu ilikuwa ni utekelezwaji wa agizo la serikali la usambazwaji wa umeme kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ambapo Mh. Waziri Mkuu alinukuliwa akisema serikali itasambaza umeme kwenye vijiji vyote vya Halmashauri ya wilaya hii kupitia mradi wa REA awamu ya III.
Kuhusu Sekta ya Elimu, Waziri Mkuu alitoa agizo kali kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya kuwarubuni watoto wa kike na kuwafanya wakatishe masomo yao ambapo alisema kwa yeyote atakayejihusisha na jambo hilo atakumbana na mkono wa sheria.
“Aidha nawaagiza maafisa Elimu (Msingi na Sekondari) kurekebisha Ikama ili kuwe na uwiano wa uoangwaji wa walimu kwenye shule za mjini na vijijini kutokana na kuwapanga walimu wengi mjini hali inayopelekea uhaba wa walimu kwenye baadhi ya shule zilizopo vijijini”, alisisitiza Mh. Wazri Mkuu.
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu alisisitiza, Hamashauri kuweka mpango mkakati katika kuhakikisha kila tarafa inakuwa na shule moja kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita.
Jambo jingine ambapo liliamsha hisia za wananchi lilikuwa ni suala la zao la kahawa ambapo Waziri Mkuu alisisitiza kwamba serikali imelenga kuimarisha zao la kahawa ikiwa ni moja kati ya mazao matano ya biashara ambayo ni ya kimkakati.
Waziri Mkuu alikemea vikali ununuzi wa kahawa kwa njia ya magendo maarufu kama ‘obutula’ na kuwashauri wakulima kuendena na mfumo wa sasa wa soko.
“Aidha niwakikishie baadhi ya changamoto zilijitokeza kwenye msimu huu wa mwaka 2018/2019 hazitajitokeza tena kwenye msimu 2019/2020 kwani minada kwa ajili ya ununuzi wa kahawa hizo itakuwa kila mkoa na hivyo kupunguza gharama ya kusafirisha kahawa kupeleka mjini Moshi ambako ndiko kwenye soko”, alisema Waziri Mkuu.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.