WATENDAJI WA NGAZI ZA CHINI “WAPIGWA MSASA”
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Mafunzo ya siku moja yaliyofanyika katika Ukumbi wa Vijana Rafiki wa Angaza, yakihusisha wataalam wa ngazi za chini wapatao 147 katika Halmashauri ya Wilaya hii yanatajwa kuwa chachu muhimu katika kuchochea ari ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mafunzo hayo yaliyotolewa kwa kada za watendaji wa Kata na Vijiji, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata, baadhi ya Maafisa Afya, Maafisa Elimu Kata na Maafisa Ugani kutoka katika Kata zilizopo katika Halmashauri hii yaliangazia mada kadhaa wa kadhaa ikiwemo Utendaji katika Utumishi wa Umma kwa kuzingatia kanuni na sheria, Maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa aliyoyatoa kwa maafisa Ugani hivi karibuni ikiwemo suala la kuisha katika maeneo ya ngazi za chini yaani kwenye vijiji na kata kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mada nyingine iliyoangaziwa katika mafunzo haya ilikuwa ni suala Ukusanyaji wa Mapato kwa kutumia Mashine (PoS), Uibuaji wa Miradi ya Maenddeleo na Usimamizi na Elimu dhidi ya Rushwa.
“Kupitia mafunzo haya hatutarajii kuona mambo yakikwama kwa sababu tu ya hulka ya baadhi ya watumishi katika ngazi za vijiji na kata kutothamini kufanya kazi kama Timu na hii imethibitika kwamba maeneo ambayo watu wamefanya kazi pasipo ushirikiano wameshindwa vibaya”, alisisitiza Afisa Elimu Msingi, Donati Bunonosi.
Aidha, kupitia kikao hicho wajumbe kwa kauli moja kupitia kikao hicho kilichokuwa chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya hii, Mh. Wallace Mashanda waliweka maazimio kadhaa ambayo yatapaswa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi sita ambapo taarifa yake ya utekelezaji inapaswa kuwasilishwa kwenye kikao kama hicho kitakachofanyika Januari 2019.
Baadhi ya maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho ilikuwa ni kwamba kufikia Septemba 2018 watendaji wa Vijiji chini ya uratibu wa kata kwa kushirikiana na Afisa Sheria wa Wilaya, Samara Matiko watunge sheria ndogo katika maeneo yao zitakazosaidia katika kuratibu shughuli mbalimbali ikiwemo kuongeza wigo katika suala la ukusanyaji wa mapato.
Maazimio mengine ilikuwa ni suala la kuhakikisha vikao vya kisheria kwa taasisi zote za ngazi za vijiji na kata vinafanyika bila kisingizio chochote, kusoma kwa taarifa za mapato na matumizi na kila ngazi ya kijiji na kata kuwa na mpango wa jumla na wa kila mwaka unaoendana na mpango wa Bajeti na Matumizi.
Aidha maazimio mengine yalikuwa ni kufufuliwa kwa kamati za kukusanya mapato kwa kila kata ili kufanikisha suala la kukusanya mapato kwenye maeneo yao ikiwa ni pamoja na suala la Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya kuwatolea nyaraka mbalimbali watendaji hao ili kuwarahisishia katika suala la utendaji wao wa kila siku.
“Katika kikao hiki ni lazima tuazimie juu usimamizi wa shughuli za kila siku bila ya kuoneana haya na kila kata itumie vikao vyote vinavyofanyika katika maeneo yao ili kuwaelimisha juu ya usahihi wa majina ya watoto wao pindi wanapowaandikisha shule”, alisisikika Mh. Mashanda akiwahoji washiriki wa mafunzo hayo.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.