WANAWAKE WAWEKA MIKAKATI YA ‘KUFA MTU’ KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA.
Na Innocent Mwalo, KARAGWE.
Wanawake wilayani hapa wameweka mikakati kadhaa ya kukabiliana na changamoto zilizopo katika jamii yao ili waweza kufikia azima ya Tanzania ya viwanda.
Hayo yalibainishwa kupitia risala yao iliyosomwa na Edina Kabyazi ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri hii kwa mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Wilaya Karagwe Mh. Innocent Nsena katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo hufanyika kila Machi 08, huku mwaka huu shamrashamra hizo kiwilaya zilifanyika katika kata ya Rugera.
“Ndugu Mgeni rasmi wanawake wilayani hapa kwa kauli moja tumedhamiria kuendelea kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuwepo kwa usawa wa kijinsia kama msingi wa maendeleo ya kiuchumi kwa kutumia raslimali zilizopo”, alibainisha Edina kupitia taarifa hiyo iliyosomwa nae kwa mgeni rasmi.
Mikakati mingine iliyotajwa ili kukabiliana na changamoto ya kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika kuelekea uchumi wa viwanda kama ilivyobainishwa katika kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka huu inayosema “Kuelekea uchumi wa viwanda, tuimarishe usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake vijijini” ilikuwa ni kusajili wanafunzi wa kike na wa kiume kwa uwiano sawa hasa katika shule za sekondari sanjari na ujenzi wa mabweni.
Aidha wanawake hawa waliweza kukubaliana juu ya mkakati wa kuongeza madarasa, madawati na kukamilisha ujenzi wa maabara kwenye maeneo ambapo kuna changamoto ya miundombinu hiyo kwa ajili ya kuboresha maeneo hayo ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya kusoma na kujifunzia.
“Tutaendelea kuimarisha Idara ya Maendeleo ya Jamii hasa Kitengo cha Jinsia na watoto kwa kuwawezesha kufanya kazi yao kwa ufanisi na kuwafikia walengwa wengi iwezekanavyo”, alisisitiza Edina.
Eneo jingine lililowekewa mkazo na wanawake hawa ilikuwa ni ajenda ya Halmashauri ya wilaya kuendelea kutunisha mfuko wa wanawake na vijana na kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa SACCOS na vikundi vya wanawake na vijana ili kuinua kipato katika familia.
Kwa upande wao baadhi ya wanawake waliohojiwa katika eneo yalipofanyika maadhimisho hayo waliupongeza uongozi wa Halmashauri ya wilaya kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi na Jamii kwa kuratibu vizuri sherehe hii iliyowakutanisha wananawake ambapo kwa pamoja waliweza kujadiliana juu ya changamoto hizo.
Naye Mgeni rasmi, Mh. Nsena aliwataka wawanake kutumia fursa zilizopo kwa ajili kujiletea maendeo ya kufikia uchumi wa viwanda.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.