WANAWAKE, VIJANA, WENYE ULEMAVU WAENDELEA ‘KUCHUMA NEEMA’ WILAYANI KARAGWE
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Uongozi wa Halmasahuri ya Wilaya Karagwe umeendelea kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. John Pombe Magufuli la kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Hayo yalijidhihirisha mapema juma hili, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Mh. Godfrey Mheluka aliweza kukabidhi hundi ya kiasi cha Tsh. 24,500,000.00 kwa jumla ya vikundi 13 vitakavyonufaika na mkopo huo ikiwa ni utekelezaji wa agizo hilo la Rais alilolitoa wakati wa uzinduzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, Novemba 2015 ambapo pamoja na mambo mengine aliziagiza Halmasahuri kote nchini kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kazi hiyo.
Vikundi vilivyonuifaika na mikopo hiyo ni NDAWOSA kutoka Kata ya Ndama, Umoja wa Vijana wa Boda Boda wa Kata ya Kihanga, Tuinuane Na. 605 na Upendo, vyote kutoka Kata ya Nyaishozi na Mkombozi Rukola kutoka Kata ya Nyakabanga.
Aidha katika orodha hiyo vilikuwepo vikundi vingine kama kile cha Tubehamo kutoka Kata ya Nyakabanga, Upendo cha Kata ya Kanoni na Kanyinya na Tuinuane VICOBA kutoka Kata ya Kibondo.
Vikundi vingine vilivyonufaika na mikopo hiyo vilikuwa ni Kazana kutoka Nyabiyonza na vile vya Mkombozi na Tuleane vyote kutoka Kata ya Rugera na SEEDO cha Kata ya Chonyonyo.
“Ninawapongeza uongozi wa Halmasahuri kwa kutekeleza kwa vitendo agizo la Mh. Rais Magulifu lakini niwaombe ninyi vikundi mnaokopeshwa mikopo hii leo hii kuhakikisha mnarejesha mikopo hiyo kwa wakati na kwa mujibu wa mikataba yenu”, alisisitiza Mh. Mheluka.
Kwa upande wake Fortunata Komugisha mmoja kati ya wanakikundi cha wanawake kutoka katika Kata ya Ndama, ameushukuru uongozi wa Halmashauri kwa kuwapa mikopo hiyo na kuahidi kwamba vikundi vya wanawake vimekuwa vikifanya vizuri katika marejesho ya mikopo hiyo kutokana na ubunifu wa wanawake wa kujishirikisha katika shughuli za uzalishaji mali katika nyanza za Kilimo, Biashara na Ufugaji.
“Natoa wito kwa makundi mengine hasa kundi la vijana kuiga mfano kutoka kwa kundi la wanawake ili waweze kuwa katika nafasi nzuri ya kurejesha mikopo hiyo kwani kwa sasa kuna changamoto ya wao (vijana) kutokurejesha mikopo hiyo”, alisisitiza Fortunata.
Naye Samson Laurian ambaye ni mweka Hazina kutoka miongoni mwa vikundi vilivyopewa mikopo hiyo ambacho ni kikundi kinachohusisha vijana waendesha Boda Boda kutoka katika Kata ya Kihanga alimhakikisha Mkuu wa Wilaya Karagwe kwamba licha ya kupewa mikopo hiyo kikundi hicho kitaifanyia kazi kwa vitendo changamoto iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya Karagwe kuhusu Boda Boda Wilayani hapa kuwa mstari wa mbele katika kukomesha ajali za barabarani ambazo nyingi kwa namna moja ama nyingine zinachangiwa na uzembe wa madereva hao.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.