Wananchi Wilayani Karagwe Washiriki Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.
Na Innocent E. Mwalo, Chanika, Karagwe.
Katika kuonesha kushiriki kwa vitendo katika sherehe miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar wananchi Wilayani hapa wameshiriki kikamilifu katika sherehe hizo zilizofanyika katika kijiji cha Runyaga kata ya Chanika huku mgeni rasmi akiwa ni Makamu wa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya Karagwe Mh. Dauson Paulo Byamanyirwohi aliyefika kumwakilisha Mkuu wa Wilaya Karagwe.
Awali katika risala yao wananchi wa kata hiyo kupitia risala yake waliweza kulielezea tukio la kijasiri la lililofanywa na wazanzibar kupitia mapinduzi hayo ya 12/01/ 1964 kama kielelezo cha kujiondoa katika utawala wa Sultani na kujiweka huru katika Nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
“Mapinduzi ya Zanzibar yaliendeshwa na kundi la waafrika wachache waliokuwa hawazidi 600 yakiongozwa na John Okello ambapo kundi hilo lililotumia silaha za jadi likihusisha askari waliokuwa wamefukuzwa kazi kwa uonevu na serikali dhalimu iliyokuwapo madarakani kabla ya mapinduzi haya”, walisema wananchi kupitia risala yao.
Kwa upande mwingine wananchi hao waliyataja maadhimisho hayo kuwa yaliyokuwa yamelenga kuwakumbusha watanzania unyanyasaji uliofanywa na sultani wa Zanzibar akisaidiwa na mwingereza kwamba yalilenga kupinga kufanyishwa kazi ngumu kwa ujira kidogo, kulipishwa kwa kodi kubwa na hata kupuuzwa kwa haki zao za msingi hali iliyosabasisha waafrika kuungana ili kudai haki zao kupitia chama cha Afro – Shiraz Party, A.S.P
Waliyataja mapinduzi haya kama chachu kwa mapinduzi ya kiuchumi yaliyofikiwa kwenye Kata ya Chanika ambapo Kata hii yenye jumla ya Vijiji 6 vya Ruhanya, Kahundwe, Chanika, Runyaga, Ruzinga na Omurulama kama vile ujenzi wa shule za msingi saba zenye jumla ya wanafunzi 4,253 na walimu 78.
Mafanikio mengine waliyoyataja yalikuwa ni ujezi wa Shule ya Sekondari ya Chakaruru ambapo kwa sasa ina idadi ya wanafunzi 250 na walimu wapatao 15.
Kuhusu sekta ya Afya, kata hii ina zahanati mbili ambazo ni Kakiro na Chanika ambapo mafanikio yaliyofikiwa ni pamoja na uhamasishaji wa wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya (CHF).
Kwa upande wake Mh. Byamanyirwohi aliwapongeza wananchi wa kata hiyo kwa hatua kubwa waliyofikia katika kujiletea maendeleo ikiwemo suala la kuongeza usajili wa wanafunzi wote wenye umri wa kwenda shule, kuhimiza ufundishaji wa wanafunzi na kuboresha miundombinu mbalimbali.
“Pamoja na changamoto kadhaa mlizozitoa naendelea kuwapongeza Idara ya Kilimo na Mifugo kwa kutekeleza majukumu yao kama ilivyosemwa kwenye risala yao”, alisema Mh. Byamanyirwohi.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.