Wananchi Wilayani Karagwe Waishukuru Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania kwa Elimu ya Uhifadhi wa Mazingira.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE.
Wananchi Wilayani Karagwe wameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kupitia Mamlaka ya Usimamizi Wanyama Pori Tanzania, TAWA kwa Elimu waliyoitoa juu ya Uhifadhi wa Mazingira kupitia ziara yao iliyodumu kwa takribani siku nne (04) kwa kipindi cha Novemba 14 -17, 2017 kwenye kata za Rugu, Nyakasimbi, Bweranyange, Nyakabanga na Nyakakika.
Shukrani hizo zimetolewa kupitia mikutano ya hadhara ya wanakijiji na wanafunzi kwa wataalamu hao kutoka TAWA ambao walikuwa ni ndugu Mohammed Mpita, ndugu David Gunda, ndugu Winifrida Mkenda(wote kutoka Malihai Club Kanda ya Mwanza), hali kadhalika alikuwepo ndugu Winnie Kweka, Afisa Wanyamapori wa Mapori ya Akiba ya Kimisi, Burigi na Biharamulo yenye makao makuu wilayani Biharamulo ambao kwa pamoja waliambatana na dereva wao ndugu Rashid George katika msafara huo uliofanikiwa kufika katika Shule za Msingi na Sekondari kwenye vijiji na shule zinazopakana na mapori ya Akiba ya Hifadhi za Burigi na Kimisi yaliyopo Wilayani hapa.
Ikumbukwe kwamba katika ziara hiyo walikuwepo pia watumishi wa Idara ya Ardhi na Maliasili Wilayani hapa ambao ni ndugu Everln Swai, ndugu Rama Masele na ndugu Sunday John, Afisa Misitu kutoka TFS Karagwe ambao kwa pamoja waliweza kuzuru na kufanya mikutano yenye lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki katika uhifadhi wa Mapori ya Akiba na utunzaji wa mazingira kwa ujumla.
Katika Kata ya Rugu, ziara iliihusisha shule ya sekondari ya Rugu, shule za msingi za Rugu, Kasheshe na Ruhita pamoja na vijiji vya Ruhita, Rugu na Kasheshe, huku katika Kata ya Nyakasimbi, mikutano ikifanyika katika shule za msingi za Kabale, Muungano, Kyanyamisa na Kahanga, shule ya sekondari Nyakasimbi huku vijiji vya Kahanga, Nyakasimbi na Muungano vikifanya mkutano wa pamoja katika kijiji cha Kahanga.
Ziara kama hiyo ilifanyika pia katika kata ya Nyakabanga kwenye shule za msingi za Chabuhora na Bwikizo, shule ya sekondari Nono na vijiji vya Chabuhora na Kanogo.
Kwa upande wa Bweranyange, mikutano hiyo ilikuwa katika shule ya Msingi Bitaraka, shule ya sekondari Kawela na kwenye kijiji cha Muguruka huku tamati ya mikutano hii ikiwa Novemba 17, 2017 kwenye kata ya Nyakakika iliyohusisha vijiji vya Kandegesho, Nyakakika, Kaiho, shule za msingi za kandegesho, Matale na Kaiho.
Katika maeneo yote wananchi wanaunga mkono elimu hii na wanaahidi kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira.
Ndugu Suniva Johabu, Ignas Innocent na Zaituni Raphael wote wakiwa ni wote wakiwa ni wakazi wa kijiji cha Rugu kwa nyakati tofauti wakisikika wakisema huenda baada ya Elimu hiyo wimbi la ujangili lipungua huku wakikiri kwamba huenda watu wengi wemejikuta wakitenda ujangili huo kwa kutokujua sheria namba 05 ya mwaka 2009 kuhusu masuala ya kuhifadhi wanyama pori.
“Kwa kweli suala la watu kutokufanya shughuli za uzalishaji au kufanya shughuli za ufugaji kwenye mita 500 imekuwa ni changamoto sana kujua kwa hiyo tunawashukuru kwa kuja kutuelimisha”, alisikika mmoja wa wananchi walihudhuria mkutano katika kijiji cha Kaiho.
Katika kukazia maarifa kuhusu katazo hilo Afisa Wanyamapori, Wilayani hapa ndugu Everln Swai aliendelea kuonya watu wasiozingatia katazo hilo na kuendelea kufanya shughuli za uzalishaji kwenye maeneo haya huku akikitaja kitendo hicho cha ukaidi wa sheria kwamba kitaweza kuwasababishia hasara kubwa wananchi hao kwa kutaifishwa kwa mifugo yao hali kadhalika kukosa kifuta jasho au kifuta machozi pindi watakapopata athali wawapo kwenye maeneo hayo.
Aidha kupitia mikutano hiyo Zamoni Didas mkazi wa kijiji cha Kahanga alitaka kujua ni wanyama gani ambao kwa mujibu wa sheria hiyo ya uhifadhi wanyamapori wananchi wana haki ya kulipwa kama wakidhurika na wanyama hao.
Katika kujibu swali Winnie Kweka aliainisha aina saba za wanyama hatari ambao ndio wameainishwa kwa mujibu wa sheria kwamba wakiharihu mazao na kusabisha athali nyingine ikiwemo kuua au kumjeruhi mtu basi kwa kufuta utaratibu wa kutoa taarifa ndani ya siku tatu kwa Afisa Mtendaji wa kijiji hicho na kukamilisha utaratibu wa kuomba kifuta jasho au machozi kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori Tanzania.
Huku akiwataja wanyama saba wanaoainishwa na sheria kwa ajili ya kifuta jasho au machozi ambao ni tembo, chui, nyati, fisi, simba, kiboko, mamba na faru, ndugu Kweka aliwaambia wananchi hao kwamba daima hakuna kifuta machozi wala jasho kinachotolewa kwa muombaji yeyote asiyefuta utaratibu ulioainishwa katika kanuni za kifuta jasho au machozi ya mwaka 2011.
Katika mikutano hiyo wananchi wengi walikuwa na shauku kubwa ya kujua faida watakayopata kwa kushiriki uhifadhi huo.
“Hivi wataalam nisaidieni sisi tutanufakaje na suala la kuhifadhi haya mapori”, aliuliza mkazi mmoja wa kijiji cha Kanogo ambaye hakupenda jina litajwe.
Katika kujibu swali hilo, ndugu David Gunda aliwaambia wananchi hao kwamba kuna faida nyingi taifa linapata kutokana na uhifadhi kama vile ajira, lakini kwa namna ya pekee aliitaja sekta ya utalii kuliongezea taifa 17% ya mapato yake huku akiitaja sekta hii kuchangia takribani 25% ya fedha za kigeni.
“Lakini mkishiriki kikamilifu katika uhifadhi huo kuna faida ya upndeleo ambayo Halmashauri za Wilaya zinazoyazunguka mapori haya zinapata asilimia 25% ya mapato yake fedha zinazoekezwa kwenye sekta ya maji, Afya na Elimu na mfano katika wilaya hii ni katika kijiji cha Ruhita katika Kata ya Rugu ambapo yamejengwa madarasa mawili, barabara na zahanati kupitia uafadhili wa mwekezaji aliyewekeza katika mapori ya akiba ya Burigi”, alinukuliwa ndugu Gunda katika mkutano huo.
Kwa upande wa walimu na waafunzi kwenye taasisi za Elimu kulikofanyika mikutano hiyo mbali na kuahidi kuipeleka elimu hiyo kwa jamii na watu wengine ambao hawakuweza kufika na kushiriki mikutano hiyo waliahidi kuanzisha Clubs za Malihai kwenye maeneo yao ili ziweze kuchochea suala la uanzishwaji wa bustani za miti na kushiriki kikamilifu katika shughuli nyingine za uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo yao.
“Tunaahidi baada ya Elimu kuanzisha Club za Malihai hapa shuleni kwetu kwa kadri mlivyotuelekeza”, alisema Mwalimu Adventina Mfunjo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Rugu.
Ziara hii imemaliza kwa mafanikio makubwa wilayani hapa kwani wananchi wamepata nafasi katika kila eneo ya kuuliza maswali kwa maafisa hawa kutoka TAWA ambao wajibu wao ulikuwa ni kutoa Elimu ili kuwajengea uwezo wananchi kuepuka athali za ukikwaji wa sheria namba 05 ya mwaka 2009 ya wanyamapori yenye zaidi ya 13 kubwa likiwa ni kwamba si ruhusa kwa mtu yeyote kuingia ndani ya pori la Akiba bila kibali cha maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa wanyama Pori Tanzania.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.