Wananchi Wilayani Karagwe Waahidi Kushiriki Kutokomeza Ujangili.
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Katika hali ya kuonesha kuelewa na kuipokea Elimu inayoendelea kutolewa kuhusu masuala ya uhifadhi wa Mapori ya Akiba na mazingira wilayani hapa, wananchi katika maeneo ya Kata za Bweranyange na Nyakabanga kwa kauli moja wamekataa kuendelea na ujangili baada ya wataalam kutoka katika Club ya Malihai, Kanda ya Mwanza na Mhifadhi kutoka Mapori ya Akiba ya Kimisi, Biharamulo na Burigi kutoa Elimu hiyo kupitia mikutano ya hadhara ya wananchi, wanafunzi na walimu katika shule za msingi na sekondari.
Mnamo Novemba 16, 2017 wataalam hao ambao ni ndugu Mohammed Mpita, ndugu ndugu David Gunda, ndugu Winifrida Mkenda (Wote kutoka katika Club ya Malihai kanda ya Mwanza), ndugu Winnie Kweka(kutoka katika Ofisi ya Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Kimisi na Burigi yenye makao makuu Wilayani Biharamulo) na dereva wao ndugu Rashid George waliambatana na wataaalam wengine kutoka Idara ya Ardhi na Maliasili Wilayani hapa ambao ni ndugu Everyn Swai na ndugu Rama Masele walifika katika maeneo ya Kata ya Nyakabanga kwenye Shule za Msingi za Chabuhora, Bwikizo, Shule ya Sekondari ya Nono na vijiji vya Chabuhora na Kanogo kwa ajili ya kutoa Elimu hiyo huku katika kata ya Bweranyange, Elimu hii ikitolewa kwenye maeneo ya Shule ya Msingi Bitaraka, Shule ya Sekondari ya Kawela na katika kijiji cha Chamchuzi.
Aidha katika msafara huo alikuwepo ndugu Sunday John, Afisa Misitu kutoka Wakala wa Misitu Tanzania, TFS hapa Karagwe, kwa ajili ya uhamasishaji wa utunzaji wa mazingira kwa kuepuka kukata miti kwa ajili ya mkaa na zaidi kuongeza jitihada katika kuhifadhi mazingira.
Kote walikupita wataalam hawa walitoa Elimu hiyo ya uhifadhi na mazingira hasa wakiwafundisha wananchi hao juu ya makatazo mbalimbali yaliyomo kwenye sheria namba 05 ya mwaka 2009 ya kuhifadhi mapori ya Akiba ya wanyama pori.
Mapema ndugu Everyn Swai akiwatambulisha wageni hao kwa wananchi alielezea faida ya kuhifadhi mapori ya akiba ya Kimisi na Burigi kwa wananchi wa Wilaya hii huku akisisitiza kwamba kama utafanyika uhifadhi wenye tija wananchi wilayani hapa wataweza kunufaika na gawio la 25% kutokana na mapato ya sekta ya utalii katika, fedha ambazo huelekezwa katika utekelezaji wa wa miradi ya Elimu, Afya na Maji, zikiwa ni kati ya sekta zenye changamoto kubwa katika Halmashauri ya Wilaya Karagwe.
Ndugu Everyn Swai aliendelea kusisitiza kwamba ufinyu wa Elimu ya uhifadhi na mazingira ni moja kati ya mambo yaliyopelekea wataalam hao kufika katika maeneo hayo kwa ajili ya kutoa Elimu hiyo ili kuwasaidia kuifahamu sheria ya kuhifadhi na wanyamapori ambayo ukiukwaji wake utapekekea wananchi wengi kukumbwa na adhabu ya kifungo cha miaka isiyopungua 20, kutozwa faini, kutaifishwa kwa mifugo inayokamatwa kwa uvamizi kwenye Hifadhi hizo za Mapori ya Akiba au vyote kwa pamoja kutokana.
Awali, ndugu David Gunda katika moja ya mikutano hiyo aliwaasa wananchi kupunguza na kuzuia migogoro na wanyamapori kwa kujifunza mbinu mbalimbali za kuzuia wanyamapori wasisabaishe madhara kwa binadamu, mazao, na mifugo yao.
“Lakini iwapo wanyamapori watasababisha madhara kwa binadamu na mali zenu; hasa uharibifu unaosababishwa na wanyama saba wanaotambulika kama wanyama hatari ambao ni tembo, nyati, fisi, samba, kiboko, mamba na faru basi serikali itatoa kifuta machozi au kifuta jasho kutokana na athali hizo kama inavyoelekezwa katika kanuni za kifuta jasho na machozi ya mwaka 2011”, alinukuliwa Gunda katika moja ya mikutano hiyo.
Kadhalika, ndugu Gunda aliwasisitizia wananchi hao kwamba kwa mujibu wa sheria hiyo ya uhifadhi, mwananchi anayeathiriwa na wanyamapori anapaswa kutoa taarifa au tukio hilo kwa Afisa Mtendaji wa kijiji wa eneo la tukio ndani ya siku tatu, na kukamilisha utaratibu wa kuomba kifuta jasho au machozi kwa Mkurugenzi wa wanyamapori.
“Hakuna kifuta machozi au jasho kinachotolewa kwa muombaji asiyefuta utaratibu ulioainishwa katika kanuni za kifuta jasho na machozi za mwaka 2011”, alisema ndugu Gunda.
Wataalam hawa waliweka mkazo kwenye makatazo kadhaa mbalimbali yaliyopo kwenye sheria ya uhifadhi yakiwemo yale yanayozuia mtu yeyote kuingia ndani ya Pori la Akiba bila kibali cha maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
“Katazo jingine ni kwamba hairuhusiwi kwa mtu yeyote kuwa na silaha yeyote ndani ya Pori la Akiba bila kibali cha maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori”, alisisitiza ndugu Winifrida Mkenda.
Makatazo mengine ni kwamba hairusiwi kuchoma moto, au kukata miti, nyasi, kuingiza mifugo, kuwinda , kukamata, kuua au kujeruhi mnyama yeyote au smaki ndani ya Pori la Akiba bila kibali cha maandishi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori.
Aidha makatazo mengine yanahusu zuio la kuingiza na kulisha mifugo, kujeruhi mifugo na kufanya uwindaji kwenye maeneo ya hifadhi za Wanyamapori.
Ziara hiyo itaendelea mnamo Novemba 17, 2017 kwa kutembelea maeneo ya Kata ya Nyakakika kwa kusudi hiyo ya utoaji wa Elimu juu ya sheria, na kanuni za uhifadhi wa Mapori ya Akiba ili wananchi waweze kufahamu sababu za kuhifadhi wanyamapori na kisha wafanikishe azma ya serikali kupata faida kutokana na uhifadhi.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.