Wananchi Wakubali Ujenzi Makumbusho ya Bweranyange kwa 99%
Na Innocent E. Mwalo, KARAGWE
Wananchi wa Kijiji cha Kijumbura Kata ya Bweranyange Wilayani hapa wamepitisha kwa asilimia 99 uamuzi wa kujengwa kwa makumbusho ya kihistoria ya kisasa katika kijiji hicho huku wakipendekeza makumbusho hayo kuitwa “Makumbusho ya kumuenzi Mkama Daud Rumanyika wa II”
Uamuzi huo wa kihistoria ulifikiwa mnamo Novemba 03, 2017 kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya Msingi Kijumbura huku mgeni rasmi akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Mh. Wallace Mashanda.
Wengine katika ujumbe huo walikuwa ndugu Alloyce Mujungu, Afisa Utamaduni ambaye pia alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ndugu Godwin Kitonka aliyeshindwa kufika katika mkutano huo kutokana na majukumu mengine muhimu, Mchungaji Dkt. Geofrey Aligawesa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mpango Mkakati wa Wilaya.
Pia alikuwepo ndugu Adam Salum, Afisa Kilimo Wilaya, ndugu Benson Abel, Afisa Ardhi wilaya, ndugu Mmasa Mmasa, Afisa vijana na waandishi wa Habari.
Kwa upande wa wenyeji, alikuwepo Afisa Tarafa ya Nyabiyonza ndugu Erasto Hajanja, Mtendaji wa Kata ya Bweranyange ndugu Nicolous Lubambula na uongozi wote wa kijiji cha Kijumbura ukiongozwa na mwenyekiti wa kijiji hicho ndugu Even Eustard.
Awali, ndugu Christian Rumanyika, Mwenyekiti wa ukoo wa Bahinda, alimmwagia sifa kemkem Afisa Utamaduni Wilayani hapa ndugu Alloyce Mujungu akimtaja kwamba ni mtu muhimu aliyeshirikiana nae toka kuasisiwa kwa wazo la ujenzi wa makumbusho hayo mwaka 2007.
“Kwa kweli ninayo furaha sana kuona sasa jambo tulilopigania kwa takribani miaka kumi na Mujungu (Afisa Utamaduni) linaenda kufanikiwa”, alisisitiza Christian Rumanyika.
Baada ya maelezo hayo ya kiongozi huyo wa ukoo, mwenyekiti wa Halmashauri, Mh. Mashanda akawauliza kwa mara nyingine wananchi hao walikuwa wakimsikiliza kwa makini kama wanaafiki uamuzi wa kujenga makumbusho hayo ambapo wananchi hao kwa takribani asilimia 99 walinyoosha mikono kuridhia uamuzi huo.
Baada ya ridhaa hiyo ya wananchi, Mchungaji Dkt. Aligawesa aliyekuwa mmoja wa wawasilishaji wa mada kwenye mkutano huo aliweza kuwaeleza wananchi hao chimbuko la ujenzi wa makumbusho hayo huku akitanabaisha kwamba mwaka 2011wakati wa maadhimisho ya siku ya utamaduni wa mnyambo yalipofanyika jijini Dar es Salaam kuliundwa kikosi kazi.
“Jukumu hilo la msingi la kikosi kazi hicho lilienda sambamba na kuzitafuta na kutunza malikale lengo likiwa kufufua utamaduni wa mnyambo”, alisema Mchungaji Aligawesa.
“Katika kutekeleza jambo hili tulilalazika kujifunza mambo kadhaa kwa wenzetu wa Uganda ambao wao bado wana mfumo wa watemi wa jadi ambao kwa kweli umekuwa kituo muhimu cha utamaduni wa utalii”, alisisitiza Mchungaji Aligawesa.
Afisa Ardhi ndugu Abel Benson aliwasilisha mada juu ya matumizi bora ya ardhi na ujenzi wa makumbusho ya Kitaifa ya Mkama Rumanyika huku akiainisha mambo kadhaa yatakayofanywa kabla ya kuanza ujenzi wa makumbusho hayo ikiwemo kuletwa kwa Afisa Mipango miji kwa ajili ya kupanga mji huu, kupimwa kwa ardhi ardhi kwa maeneo ya kata ya Bweranyange lakini hasa vijiji vya Kijumbura yalipo Makumbusho hayo na Bweranyange yalipo maziko ya wakama.
“Jambo jingine linalotakiwa kutekelezwa ni kuwepo kwa masjala ya ardhi”, alisema ndugu Abel.
Huku akisisitiza faida za upimaji wa ardhi, Abel alisema” upimaji wa ardhi utasaidia sana katika kupunguza migogoro ya ardhi katika maeneo haya” alisema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bweranyange, Mh. Fidelis Berere alitumia muda huo kusisitiza kwamba wananchi wa kata yake hawajawahi kukataa mradi wowote pindi unapoletwa na serikali.
Naye mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Kata hii, ndugu Cosmas France na baadhi ya wananchi kadhaa waliopata wasaa wa kuzungumza waliridhia ujenzi wa makumbusha na kuwasihi wananchi wengine kuridhia pia.
Wananchi hao waliopata nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya wengine walikuwa ndugu Katani Abel Kashau, ndugu Daud Ruhinda, ndugu Peter Kamanzi na ndugu Innocent Kamanzi huku kwa kiasi kikubwa kila mmoja akiridhia wazo hilo lakini wengine wakatahadharisha kutenganishwa kwa eneo la makumbusho na maeneo mengine ya kilimo ili kuepusha migogoro ya ardhi hapo baadae.
Mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, Mh.Mashanda alianza kwa kuwashukuru wananchi hao kwa mahudhurio mazuri na kwa kukubali mradi huu akitanabaisha kwamba upimaji wa ardhi utawawezesha wananchi hao kumiliki ardhi hai itakayowawezesha pamoja na mambo mengine kuwa na hati ya ardhi iliyopimwa itakayowezesha kukupeshwa na taasisi za kifedha ikiwemo benki.
Mh. Mashanda alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi hao kutoweka vikwazo katik ujenzi wa mradi huo lakini akasisitiza kama kuna haki wananchi wanapaswa kuipata kupitia kupisha ujenzi wa makumbusho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya aizingatie.
“Kutakuwa na gharama za upimaji wa ardhi lakini niwaombe wananchi wa kijiji hiki kukaa na wataalam toka wilayani wanaohusika na upimaji wa ardhi ili kuwepo na mwitikio mkubwa wa watu kwani kama kutakuwa na mwitikio mkubwa basi gharama zitapungua”, alisisitiza Mh. Mashanda.
Kupitia mkutano huo, Mh. Mashanda alimwagiza ndugu Mujungu kuhakikisha mihutasari ya vikao vyote vilivyoketi kufikia uamuzi huo wa ujenzi wa makumbusho upelekwe ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya na Idara ya Ardhi ielekezwe kufanyia kazi taarifa hizo.
Baada ya hapo Mh. Mashanda alisisitiza mambo kadhaa kupitia ambayo yalihusu uhamasishaji wa wananchi kulima zao la alizeti huku akiwaasa kuwa kuna viwanda takribani saba wilayani hapa vinavyohitaji malighafi hiyo.
Pia Mh. Mashanda alihimiza ulimwaji wa zao la parachichi ambalo alilitaja kama zao ambalo hizi karibuni limeongeza thamani ya uzalishaji baada ya kupatikana kwa mnunuzi wa zao hilo kwa ajili ya utengenezaji wa bidhaa kama vile vipodozi.
Kuhusu suala la Elimu, Mh. Mashanda alikubaliana na wazazi hao na kuweka mikakati kadhaa ili wanafunzi wa Shule ya msingi Kijumbura ikiwa ni shule pekee kati ya shule tano za msingi katika kata ya Bweranyange ambayo wanafunzi wake hawanywi uji.
Kupitia Mkutano huo, Mh. Mashanda alikubaliana na wananchi hao kwamba jitihada zifanyike hasa baada ya kuvuna mwishoni mwa mwezi Januari, 2018 ili wanafunzi hao waweze kunywa uji.
Aidha Mh. Mashanda aliwapongeza wazazi katika kata hiyo kwa uamuzi wao mzuri uliowawezesha wanafunzi wote wa Shule ya Sekondari Kawela iliyopo kwenye kata hiyo kuishi bwenini hali aliyoitaja kwamba itachochea maendeleo ya kitaalum kwa wanafunzi hao.
Mh. Mashanda alisisitiza na kuonya juu ya suala la uchomaji wa moto huku akiitaja kata ya Bweranyange kama moja ya maeneo yenye kesi a uchomaji wa moto kwa mwaka 2017 lakini akaonya jambo hili lisirudiwe wakati ujao kwani sheria kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakaye kwenda kinyume na agizo hilo.
Agizo jingine lilikuwa suala la upandwaji wa miti rafiki aina ya mitoma kwenye milima yenye vipara hali iliyojionesha pia kwenye vilima vya Kijumbura ili kuweza kulinda ikolojia ya milia hiyo.
Kadhalika Mh. Mashanda aligusia suala la maambukizo ya UKIMWI na kutoa ushauri kwa wananchi kujihadhari na ugonjwa huu kwa kuwa na mpenzi mmoja ama kusubiri kwa wale ambao hawajaoa aidha kutumia kondom pale wanaposhindwa kuzingatia jambo la kuwa na mpenzi mmoja na kusubiri.
KARAGWE KAGERA TANZANIA
Anuani ya posta: BOX 20 KARAGWE
Simu: 028-2227148
Simu ya mkononi: 028-2227148
Barua pepe: ded@karagwedc.go.tz ded.karagwedc@kagera.go.tz
Copyright©2017 karagwedc. All rights reserved.